Mgombea aahidi kuanza na elimu


Muktasari:

  • Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Kituo cha Mabasi Sanya mjini, Mosi alisema atashirikiana na wana Siha katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha kwa tiketi ya Chadema, Elvis Mosi amesema moja ya kipaumbele chake endapo atachaguliwa ni kuhakikisha anaboresha elimu itakayowawezesha wana Siha kutatua changamoto zinazowakabili.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Kituo cha Mabasi Sanya mjini, Mosi alisema atashirikiana na wana Siha katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili.

Akimnadi mgombea huyo, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema Mosi ndiye mgombea sahihi atakayelinda na kutetea masilahi ya wana Siha na ni mtu asiye na tamaa wala uchu wa madaraka.

Wakati Mosi akitoa ahadi ya elimu, mpinzani wake kwa tiketi ya CCM, Dk Godwin Mollel alisema akipewa tena ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha wafugaji wanapata maeneo ya malisho.

Pia aliahidi kumaliza mgogoro wa eneo la Kia na kushughulikia upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.

Alisema zipo changamoto zinazolikabili jimbo hilo ambazo alishindwa kuzitafutia ufumbuzi akiwa mbunge kwa tiketi ya Chadema, lakini kwa sasa ataweza kuzishughulikia nazo kwa kuwa yupo CCM, chama ambacho alisema ni cha maendeleo.

Akiwa katika vijiji vya Ormelili na Donyomurwak, Dk Mollel alisema maeneo hayo yanakabiliwa na tatizo la umeme na zahanati na akishinda atashirikiana na Serikali kumaliza adha hizo.

Katika Jimbo la Kinondoni, mgombea wa Chadema, Salum Mwalimu aliwaomba wananchi wa huko kumpigia kura Jumamosi ijayo ili awatumikie kwa miaka mitatu.

Akiwa Makanya Ndugumbi alisema, “Tafadhali naomba kura zenu naomba utumishi wa miaka mitatu nikawawakilishe bungeni.”

Alisema kazi ya mbunge ni kusimamia haki na mahitaji ya wananchi. “Haki za bodaboda, mamalishe, madaktari na watu wote nitazisimamia iwapo nitachaguliwa.”

Alisema jimbo hilo lina makazi yasiyo bora, yasiyo na mifereji ya kupitisha maji hali inayosababisha maradhi kama kipindupindu jambo aliloahidi kulifanyia kazi.

Alisema akichaguliwa kuwa Mbunge hakuna atakayehamishwa kupisha mradi wowote kabla hajalipwa fidia.

Mgombea mwingine katika jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Maulid Mtulia akijinadi katika Uwanja wa Kigogo People, alitoa sababu mbili za kuchaguliwa kuwa mbunge.

Alisema ni mgombea aliyepitia tiketi ya CCM chama kilichopewa ridhaa ya kuongoza nchi na kupata Rais wa Tanzania. Pia alisema chama hicho kimepewa ridhaa ya kukusanya kodi, kupanga mipango pamoja na bajeti.

“Nilikuwa mbunge wenu kwa miaka miwili, shida zenu zilikuwa zangu, matatizo yenu yalikuwa yangu,” alisema Mtulia ambaye alikuwa mbunge wa Kinondoni kabla ya kujivua uanachama wa CUF na kuhamia CCM mwishoni mwa mwaka jana hivyo kupoteza kiti hicho.

Alitoa ahadi kwamba atahakikisha mifereji ya majitaka inajengwa kwa kutumia mfumo wa kisasa hasa mawe, ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme wa sola ili kupunguza gharama za nishati hiyo jimboni humo.

“Tunaenda kutoa mikopo kwa vijana wa bodaboda na watarejesha katika mfumo mzuri wakati wakiwa wanajiendeleza,” alisema Mtulia.

Mgombea CUF, Rajabu Salum akiwa Makumbusho mchangani alisema, “Mkinichagua moja ya mambo ambayo nitayafanya ni kuhakikisha watoto shule wanapata mlo walau wa siku moja. Pia nitaondoa ada za uchukuaji maiti katika hospitali zetu kwa kuwa zimekuwa mzigo kwa wananchi.”

Pia aliahidi kuondoa kero ya maji na kuhakikisha uwepo wa bajeti kwa ajili ya matibabu bure kwa wanawake na watoto.

Bakari Kiango, Raymond Kaminyonge, Nasra Abdallah, Eliza Edward, Fortune Francis, Aurea Semtowe (Dar) na Flora Temba (Moshi).