Mgombea ataka kura za ndiyo

Muktasari:

  • Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni ya chama hicho kwenye Kijiji cha Nangwa juzi, Daffi aliwaomba wananchi wasihadaike kwa lolote na kupoteza kura zao.

Mgombea udiwani wa Kata ya Nangwa wilayani Hanang Mkoa wa Manyara, Yohana Daffi (Chadema) amewataka wananchi wa eneo hilo kwa kumpigia kura nyingi za ndiyo ili chama hicho kiendelee kuongoza kama awali.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni ya chama hicho kwenye Kijiji cha Nangwa juzi, Daffi aliwaomba wananchi wasihadaike kwa lolote na kupoteza kura zao.

Alisema wakazi wa Nangwa wanapaswa kuonyesha hisia zao kwenye sanduku la kura kwa kuikataa Serikali ya CCM kwa kumchagua mgombea wa Chadema.

Daffi alisema ili kuonyesha kuwa wamedhamiria kuendeleza ushindi wa Chadema kwenye kata hiyo wananchi wamchague ili awe diwani.

Alisema ukandamizaji unaofanywa na CCM, ikiwamo kuwa na maisha magumu, unyanyasaji na kukatazwa kufanyika mikutano ya hadhara, unapaswa kuonyeshwa kwa kuinyima kura.

“Wananchi wa Nangwa wanamsimamo thabiti unaowapa uamuzi wa kumchagua mtu wanayemtaka wao, nawaahidi tupo pamoja,” alisema Daffi.

Aliwaahidi utumishi uliotukuka pindi wakimchagua kuwa diwani wao kwa kuhakikisha changamoto zinazowakabili anazifikisha kwenye halmashauri ya wilaya hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili (Chadema) alisema ana imani kubwa na wananchi wa Nangwa kuwa wataipa heshima Chadema kwa kumpigia Daffi kura nyingi za ndiyo.

“Wananchi tunawategemea mno katika kutetea demokrasia yenu kwa kuichagua tena Chadema ili iendelee kuwa sauti ya eneo hili kwenye halmashauri ya wilaya,” alisema Kamili.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bryceson Kibassa wagombea udiwani wa kata hiyo watakaopambana kwenye kinyan’ganyiro hicho kinachorajia kufanyika Novemba 26 ni Portagia Baynit (CCM), Yohana Daffi (Chadema) na Lucy Sulley (CUF) .

Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, mgombea wa Chadema alishinda kata hiyo kwa kupata kura 1,452 CCM (1,347), ACT (nane) na CUF kura sita.