Mgombea udiwani CCM adai nyumba yake imechomwa moto

Muktasari:

  • Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Julai 15, 2018 Mlimba amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, kubainisha kuwa aliamshwa na mkewe baada ya kusikia watu wakimwaga maji katika dirisha la chumba chake.

Tunduma. Wakati kampeni za uchaguzi wa marudio katika jimbo la Buyungu na kata 77 zikianza leo Jumapili Julai 15, 2018, mgombea udiwani wa CCM kata ya Mwaka Kati, Ayoub Mlimba amesema amenusurika kifo  baada ya watu wasiojulikana kuchoma nyumba yake moto

Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Julai 15, 2018 Mlimba amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, kubainisha kuwa aliamshwa na mkewe baada ya kusikia watu wakimwaga maji katika dirisha la chumba chake.

“Niliamka ili kujua ni kitu gani kilichomwagwa dirishani lakini niliposogea ghafla ulitokea mlipuko kama bomu huku ukiambatana na moto. Hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kutafuta namna ya kujiokoa,” amesema.

Amesema wakati mkewe akikimbilia vyumbani kwa ajili ya kuwaokoa watoto, yeye alikwenda kuomba msaada kwa majirani.

“Nilipofanikiwa kufungua mlango, nilianza kupiga kelele nikiomba msaada kwa majirani. Katika harakati za kuzima moto nilidondoka na sehemu ya miguu yangu iliungua na moto,” amesema.

“Polisi walifika eneo la tukio na nyuma ya nyumba yangu walikuta madumu mawili, moja likiwa na mafuta nusu na jingine likiwa limejaa. Ni mafuta ya petroli yaliyochanganyika na dizeli, pia kulikuwa na kipande cha nondo na kopo kubwa la maji.”

Amehusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa, akidai hilo ni tukio la pili kwake tangu alipojivua udiwani wakati akiwa mwanachama wa Chadema na kuhamia CCM, Februari mwaka huu.

MCL Digital ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amesema hawezi kutoa ufafanuzi wa suala hilo kwa njia ya simu.