Mgombea udiwani Sau asimulia alivyopigwa baada ya mkutano

Muktasari:

  • Kisuguru ambaye aliwahi kugombea udiwani Kata ya Pemba kwa tiketi ya Sauti ya Umma (Sau) alisema kabla ya Krismasi watu walienda nyumbani kwake Mtaa wa Buyuni uliopo Kata ya Pemba, wakamuita naye akawafuata barabarani.

 Wakati wengi wakiwa na kumbukumbu nzuri kwa namna walivyosherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kuukaribisha mwaka mpya, mwanasiasa Mahadh Kisuguru anaendelea kuuguza majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu watano.

Kisuguru ambaye aliwahi kugombea udiwani Kata ya Pemba kwa tiketi ya Sauti ya Umma (Sau) alisema kabla ya Krismasi watu walienda nyumbani kwake Mtaa wa Buyuni uliopo Kata ya Pemba, wakamuita naye akawafuata barabarani.

Alisema alipowafuata na kuwafikia walimuuliza, ‘kwanini huwaheshimu viongozi wako?’ lakini kabla hajajibu wakaanza kumshambulia maeneo mbalimbali ya mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyomfanya apelekwe hospitali kwa matibabu.

“Walinipiga wakanijeruhi. Hawakunipa nafasi ya kujieleza. Waliendelea kunishambulia ila kwa bahati nzuri akapita mjumbe wa mtaani kwangu, Hamis Jasho ambaye aliwasihi waniache, walimsikiliza lakini wakanipa onyo,” alisema Kisuguru .

Alisema amefungua kesi ya kujeruhi yenye namba KGD/IR/73261/2017 Kituo cha Polisi Kigamboni ambako uchunguzi unaendelea.

“Shambulio hilo limepandisha presha na kisukari. Mara nyingi nalazimika kupumzika ili kutuliza afya. Sikukuu zote zimenipita,” alisema.

Kabla ya tukio hilo, alisema alitoa mchango wake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusikiliza kero za wananchi ndiko kulikomsababishia masahibu hayo.

Alisema kwenye mkutano huo, alipata wasaa wa kuchangia na akamueleza mkuu huyo kuwa kwa muda mrefu wananchi wa kata hiyo wamekuwa hawapati maji baada ya tanki lililopo kutoboka hivyo kutokuwa na uwezo wa kutunza na kusambaza maji kama inavyotakiwa.

Kisuguru alisema mkuu huyo wa mkoa aliuliza ni kiasi gani kinahitajika kurekebisha tatizo hilo ili huduma zirejeshwe kama zamani.

Alisema mwenyekiti wa mtaa huo, Shaaban Shaha alisema zimebaki Sh500,000 kukamilisha gharama zote za kurekebisha tatizo lililopo.

“Mkuu wa mkoa alishangaa akasema haiwezekani wananchi wakose maji kwa kukosa kiasi hicho. Alitoa mfukoni mwake Sh500,000 na akamkabidhi mwenyekiti. Kuunga mkono juhudi hizo nami nilichangia Sh300,000,” anakumbuka.

Alisema katika mkutano huo kuna kiongozi alimwambia atamkomesha kutokana na kuiaibisha Serikali ya Mtaa kwa mkuu wa mkoa, hivyo kuyahusisha maneno hayo na kilichomtokea kabla ya sikukuu za mwisho wa mwaka 2017.

Hata hivyo, mwenyekiti Shaha alipoulizwa kama anafahamu kushambuliwa kwa mwananchi wake huyo alikiri ingawa alisema hilo ni suala la kifamilia hivyo wanaoweza kueleza ni ndugu zake (Mahadh).

“Mimi si msemaji wa familia hiyo isitoshe yeye mwenyewe ni mzima anaweza kulizungumzia hilo. Sikuwapo siku aliyovamiwa ila nilijulishwa kwa kuwa walikuwa wanataka barua,” alisema Shaha.