Sunday, November 19, 2017

Mgombea udiwani aahidi neema ya soko

 

By Happy Lazaro, mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Arusha. Mgombea udiwani wa Kata ya Muriet kupitia Chadema, Simon Mosses ameahidi kukarabati soko la eneo la Kwa Mrombo ambalo ni tegemeo la wananchi wengi.

Amesema  hayo jana Novemba 18  wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Stand  ya Mrombo na kuahidi wananchi hao kubadilisha Kata hiyo endapo watamchagua.

Amesema  kuwa, soko hilo la Kwa Mrombo linahitaji kukarabatiwa ili liweze kuwa la kisasa zaidi na kuwezesha kutoa huduma nzuri kutokana na kuwa na miundombinu mizuri na ya kisasa.

Mosses amewataka wananchi hao kumchagua yeye ili aweze kuanza na kipaumbele hicho katika kata hiyo kwa kulisemea suala  hilo katika baraza la madiwani ili waweze kutenga fungu kwa ajili ya kukarabati soko hilo.

Alisema soko hilo limekua  likikabiliwa na changamoto mbalimbali ya miundombinu  kwa kipindi cha muda mrefu Sasa.

Aidha Mosses amewataka wananchi hao kumchagua ili aweze kutatua changamoto kubwa ya maji iliyopo katika eneo hilo ambayo imekuwa ni kero kubwa na kuwafanya wananchi wa Kata hiyo kutafuta maji umbali mrefu, hivyo aliwataka kumchagua yeye ili aweze kutatua kero hiyo.

Pia ameahidi kuboresha miundombinu mbalimbali ya barabara katika Kata hiyo ili kuhakikisha inapitika vizuri hasa kipindi cha mvua ambacho kimekuwa ni changamoto kubwa kwa barabara nyingi kutopitika kutokana na kuwepo kwa matope.

"Jamani naombeni Sana mnichague Mimi ili niweze kutekeleza ahadi zote kwa  haraka na Kwa vitendo tena kwa kipindi cha  muda mfupi pindi tu nitakapochaguliwa kuwa diwani wenu hapo ndipo mtaona juhudi zangu. "amesema Mosses.

-->