Mhagama ataka sera, sheria zitizamwe upya

Muktasari:

Amesema katika kujenga uchumi wa viwanda ni muhimu jambo hilo likafanyika

 

 Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema katika kujenga uchumi wa viwanda bado Serikali inatakiwa kutazama upya sheria na sera.

Akizungumza leo Mei 25, 2018 jijini Dodoma katika mkutano wa kuhamasisha ushiriki wa wazawa katika uchumi wa viwanda, Waziri Mhagama amesema anasimamia kikamilifu suala hilo.

Amesema kila sheria inayopita bungeni amekuwa akiuliza maudhui ya ushiriki wa wazawa kwenye sheria yenyewe ama kwenye kanuni.

“Kwa sababu msingi ukiwekwa katika sheria ni lazima kanuni itafsiri jambo hilo vizuri. Sisi kama Serikali utayari wetu ni mkubwa sana,”amesema.

Amesema dhana ya ushiriki wa wazawa itakapotekelezwa katika miradi mikubwa inayofanywa na watu kutoka nje ya nchi lazima Watanzania watapata ujuzi.

“Ninaiona Tanzania mpya kupitia mkakati Local content mnaokwenda kuitayarisha. Naisubiri kwa hamu. Sera za namna hii zikitekelezwa zitachangia kukuza viwanda na makampuni ya ndani ya nchi yetu,”amesema Mhagama.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC), Being’I Issa ambao ndio waandaaji wa mkutano huo wakishirikiana na Taasisi ya Uongozi amesema bado bidhaa zinazouzwa kwa wawekezaji nchini ni chache.

Pia amesema ushiriki wa wazawa wengi katika miradi mikubwa bado ni kwenye ujuzi wa chini na hivyo kutaka kujengewa uwezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi Nchini, Joseph Semboja ametaka uwezeshaji wa wazawa ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na miradi mikubwa nchini.