Mhasibu kizimbani akidaiwa kumtukana JPM

Muktasari:

Wakili wa Serikali, Leonard Challo alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa Agosti 6 mshtakiwa akijua kuwa ni makosa, aliwasilisha ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais Magufuli kwa njia ya WhatsApp kwenye kundi la jamii liitwalo STJ Staff Social Group.

Dar es Salaam. Mhasibu wa Sekondari ya Mtakatifu Joseph, Elizabeth Asenga (40), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la kutuma ujumbe wa kumkashifu Rais John Magufuli kupitia mtandao wa WhatsApp.

Wakili wa Serikali, Leonard Challo alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa Agosti 6 mshtakiwa akijua kuwa ni makosa, aliwasilisha ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais  Magufuli kwa njia ya WhatsApp kwenye kundi la jamii liitwalo STJ Staff Social Group.

Challo alidai kuwa mshtakiwa huyo aliandika ujumbe usemao: “Godmorning humu. Hakuna rais kilaza kama huyu wetu duniani, angalia anavyompa Lissu umashuhuri, f** lile, picha yake ukiiweka ofisini ni nuksi tupu. Ukiamka asubuhi, ukikutana na picha yake ya kwanza siku inakuwa mkosi mwanzo mwisho.”

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ukadai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba ipangwe tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shaidi alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili, kila mmoja atasaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh2 milioni. Alikamilisha na kuachiwa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 22.