Mheshimiwa Temba mpya huyu hapa

Muktasari:

Temba ambaye alifunga ndoa miaka tisa iliyopita, anasema anashukuru tangu ameoa na kuwa na familia ya watoto wanne imembadili kimaisha.


Kundi la TMK wanaume, ni moja ya wasanii waliofanya vizuri miaka ya 2002 katika muziki wa Bongo Fleva.

Kundi hilo lililokuwa na mastaa wa muziki kama Juma Nature, Chege na Temba, baadaye liligawanyika na kuzaliwa makundi ya Wanaume Family na Wanaume Halisi.

Katika Makala hii mwandishi amefanya mahojiano na mmoja wa wasanii hao, Mheshimiwa Temba kujua harakati zake mbalimbali za kimuziki zilivyo kwa sasa baada ya ukimya mrefu na mikakati yake.

Msanii huyu alishawahi kutamba na vibao mbalimbali ikiwemo Nipe Mimi, Enzi Zetu, Nampenda Yeye, Nawachanganya na nyinginezo.

Katika maelezo yake Temba anasema ukimya wake ulitokana na kuwa shule, ambapo alikuwa anasomea masuala ya ukaguzi wa bidhaa za bandarini ngazi ya shahada katika chuo cha Bandari Jijini Dar es Salaam.

Temba ambaye jina lake halisi ni Amani Temba, anasema elimu hiyo alianza kuipata katika ngazi ya cheti, lakini kutokana na kiwango hicho kidogo cha elimu aliona vema akaongeza ujuzi kwa kuendelea na Shahada.

“Ndio maana kwa mwaka jana nilikuwa kimya sana hata kuachia nyimbo ilikuwa tabu, kwani mbali na kumalizia masomo yangu pia nililazimika kwenda kufanya elimu ya vitendo hivyo ingekuwa ngumu kuchanganya mambo yote kwa wakati mmoja.

“Hata hivyo nashukuru kwa sasa nimemamaliza kwani wakati nikiendelea kusaka kazi pia nimerudi katika kazi yangu ya muziki, na hivi karibuni natarajia kuwa zirani nchini London kwa mwaliko na baadhi ya wanamuziki wenzangu akiwemo Chege.”anasema.

Analionaje soko la muziki

Temba anasema kiujumla bado soko la muziki halijakaa sawa hususani katika masuala ya usambazaji na ndio maana imekuwa ngumu kwa wengi kutoa albamu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Msanii huyu anasema ili albamu yako ifanye vizuri kwa sasa unahitaji kuifanyia matangazo ya hali ya juu na kama hauna hela inaweza ikawa ngumu kwako na ndio maana watu wanaishia kuachia nyimbo moja moja ambazo ndizo zinazowapa dili la kufanya shoo.

Ili kuondokana na hili, ameomba serikali iangalie namna nzuri ambayo wasanii wataweza kufaidika na jasho lao badala ya kuishia kwenye mazungumzo ya mdomoni.

Pia anashauri kuwepo kwa ushirikishaji wa karibu kati ya mamlaka zinazojishughulisha na Sanaa na wasanii wenyewe ili kuepuka mivutano isiyo ya lazima.

“Unajua sisi tunapambana kivyetuvyetu katika kazi zetu hizi, sasa anapokuja mtu baadaye anakuwekea masharti ambayo hujui hata yametokea wapi kwa kuwa hukushirikishwa ndipo pale watu wanapokuwa wakali na kuonekana hawana adabu, ni vizuri mamlaka zikajirekebisha katika hili ili kuepuka lawama.

Anawazungumziaje wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa

Temba anasema kuna kila sababu ya wasanii kama wao waliotangulia kwenye muziki kuwakubali wasanii wa sasa badala ya kuwaonewa wivu na kuingia nao kwenye ugomvi.

Anasema kama kuna msanii anajiona kachuja hawezi kuendana na kasi ya waliopo sasa ni bora akafuata nyayo zao bila kuona aibu ikiwemo kwenye suala la staili ya uimbaji, uvaaji na namna wanavyojiweka katika kuutangaza muziki wao.

“Kwangu bifu na wasanii wanaoibukia kwa sasa na kufanya vizuri, hakuna maana, tuangalie sisi wa zamani wapi tunakosea tunashindwa kwenda na kasi yao badala ya kuingia nao kwenye ugomvi ambapo wengi ni wadogo zetu na walikuwa wakitufuatilia na kutamani kuwa kama sisi wakati tunawika,”anasema

Maisha ya kifamilia

Temba ambaye alifunga ndoa miaka tisa iliyopita, anasema anashukuru tangu ameoa na kuwa na familia ya watoto wanne imembadili kimaisha.

“Unajua zamani nilikuwa nafanya mizunguko isiyo na maana baada ya kumaliza shoo na wakati mwingine nilirudi hata asubuhi, lakini kwa sasa hivi siwezi kufanya hivyo kutokana na kuwa nina mtu nyumbani na nisingependa kumuudhi katika hilo.

“Pia kasi ya kutafuta hela na kuwa na nidhamu nayo imeongezeka, kwani kuna wanaosubiri kulipiwa ada, kuvaa na kuishi maisha mengine ambayo yote bila hela huwezi kuyafanikisha,”anasema.

Ujio wake

Amesema baada ya kimya hicho cha mwaka mmoja anatarajia kuachia wimbo mmoja ndani ya mwaka huu ambao upo katika albamu yake ya Maradhi, Ufisadi na Ujinga na kuwataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula.