Mhubiri Zimbabwe ashtakiwa, atiwa kizuizini

Muktasari:

  • Aponzwa na mkanda wa video aliousambaza mitandaoni Jumamosi
  • Asomewa mashtaka ya kutaka kupindua serikali na awekwa kizuizini
  • Mwanasheria wake apanga kwenda Mahakama Kuu kukara rufaa

Mhubiri machachari nchini Evan Mawarire aliyekamatwa juzi alishtakiwa jana mchana kwa kutaka kuipindua serikali iliyoko madarakani kikatiba kabla ya kuswekwa ndani kwa muda usiojulikana.

Mashtaka hayo yanatokana na video ambayo mhubiri huyo aliisambaza kwenye mitandao ya jamii Jumamosi ikizungumzia kuzorota kwa hali ya uchumi wa Zimbabwe. Katika mkanda huo wa video, Mawarire anasema, "Vitu nchini Zimbabwe vimeanza kuwa vya haraka."

Aliongeza: "Tumeanza kukabiliwa na hali sawa na tuliyokuwa nayo mwaka 2008. Ukosefu wa vitu umeanza kujitokeza. Katika taifa la kawaida watu hawapaswi kuwa na hofu yoyote. Tunapaswa kuishi kwa amani katika nchi yetu," alisema.

Vilevile Mawarire amewahimiza polisi kutomkamata katika kipindi chote cha mkanda wa saa moja akisema ana haki za kikatiba kuwahutubia wananchi kuhusu kudorora kwa uchumi.

Mwanasheria Harrison Nkomo wa asasi ya Sheria na Haki za Binadamu Zimbabwe aliliambia gazeti la New Zimbabwe juzi jioni kwamba alitarajia kwenda leo Mahakama Kuu kukata rufani dhidi ya hatua ya mteja wake kuwekwa kizuizini.

"Wamemkamata na kuweka ndani na hawajatupatia siku ya kufika mahakamani hivyo kesho (leo) nitakwenda Mahakama Kuu kukata rufani,” alisema Nkomo.

Mawarire alikamatwa na polisi wenye silaha wakati wa ibada.