LULU HASSAN: Mhudumu wa ndege aliyekimbilia utangazaji

Lulu Hassan

Muktasari:

Mwanamke huyu hutangaza kipindi cha Nipashe Wikiendi mwishoni mwa juma.

“Hujambo mtazamaji, karibu katika Nipashe Wikendi, jina langu ni Lulu Hassan”. Haya ni maneno yaliyozoeleka miongoni mwa watazamaji wa kituo cha televisheni cha Kenya, Citizen kutoka kwa mtangazaji Lulu Hassan.

Mwanamke huyu hutangaza kipindi cha Nipashe Wikiendi mwishoni mwa juma.

Lulu, ambaye hutangaza kipindi hiki akishirikiana na Kanze Dena, ana historia ndefu. Akizungumza na Idara ya digitali ya Cititzen Tv, Sarah anazungumza mengi ambayo mashabiki wake hawayafahamu.

Ana asili ya Seychelles

Wengi hudhani ni Msomali, mwenyewe anasema hana uhusiano wowote na jamii hiyo. Baba yake alikuwa na asili ya Seychelles na mama yake alikuwa mchanganyiko wa Seychelles na Kikuyu.

Ni mtoto wa kwanza kati ya watatu na kwamba alilazimika kuwalea wadogo zake baada ya mama yake kufariki mwaka 2007.

“Ingawa nilikuwa wa kwanza kuzaliwa sikupata taabu kuwalea wadogo zangu hata baada ya mama kufariki kwa sababu alituachia mali, binafsi nimesoma shule tu kwa walioishi Mombasa wanajua Aga Khan Academy ilivyo ya hadhi ya juu,” anafafanua.

Alisomea uhudumu wa ndege

Kabla ya kuingia kwenye uandishi wa habari alisomea masuala ya uhudumu wa ndege lakini alifungia vyeti ndani na kutafuta kazi ya utangazaji.

“Nilipopata kazi ya kutangaza redio niliona siyo vibaya nisomee masuala ya uandishi, nikarudi chuo kutafuta ujuzi,” anasema Lulu.

Alikuwa mtangazaji wa Kiingereza

Miaka nane iliyopita, Lulu alikuwa maarufu mjini Mombasa akiwa mtangazaji katika kituo cha Redio Salaam. Hakupata umaarufu kwa kutangaza kwa Kiswahili bali Lugha ya Kiingereza.

Ilikuaje akahamia kwenye TV?

“Nilipokuwa Redio Salaama, mpiga picha wa kituo cha KTN alinifuata na kuniambia nijaribu kuomba nafasi kwa kuwa watangazaji wawili wa kike wanakwenda kujifungua hivyo anahitajika mtu wa kuchukua nafasi, nilijaribu na kufanikiwa,”

Alipata ajali mbaya mwaka 2010

Akiwa bado mtangazaji katika Kituo cha KTN alipata ajali ya gari na kuvunjika mguu wa kushoto. Mpaka sasa mguu haujapona.

Umaarufu haumvimbishi kichwa

Watu wengi hubadilika wanapopata umaarufu na kuona kuna vitu wanaweza kufanya na vingine hawawezi lakini kwa Lulu ni tofauti.

“Sioni tofauti yangu na mtu mwingine ambaye siyo maarufu, nyumbani kwetu mtu anaweza kunituma dukani na nikaenda bila kujali umaarufu wangu,” anasema Lulu.

Alikutana na mumewe kazini

Lulu ameolewa na mtangazaji Rashid Abdalla aliyekuwa mtangazaji wa QTV, ndoa iliyofungwa hivi karibuni. Abdalla anasema alivutiwa na mwanamke huyo miaka 10 iliyopita alipokuwa akimsikia na kufanya jitihada za kuonana.

Alifanya harusi kubwa

Harusi yake ilikuwa ya kukata na shoka kwani majirani zake hawakupewa kadi. Kila aliyekuwa na uwezo wa kusogea eneo la tukio alifika kula na kunywa.

“Wageni wengi sikuwajua, walikuja mamia, nilifarijika kuona kuna watu wananipenda na wameamua kushiriki katika siku yangu kuu,” anasema Lulu.