Monday, December 11, 2017

Miaka 18 bila kifo cha mjamzito Kijiji cha Uturo mkoani Mbeya-VIDEO

By Syriacus Buguzi, Mwananchi sbuguzi@mwananchi.co.tz

Mbeya. Ni asubuhi katika kijiji cha Uturo, wilayani Mbarali mkoani Mbeya. Nawasili kijijini hapa na kukuta kila mkazi ameshikilia zana za kazi; akina mama wakiwa wamebeba ndoo zilizojaa udongo na mawe, vijana wakiendesha trekta ndogo (power tillers), akina baba na wazee nao wakiwa wamebeba chepeo na majembe wakichota udongo na mawe na kufukia mashimo ya barabara iliyoharibika.

Hainichukui muda mrefu kutambua kuwa juhudi hizo zinatokana na hofu mpya baada ya kijiji hicho kutokuwa na kifo cha mjamzito kwa takribani miaka 18 iliyopita. Hofu imetanda.

Hofu yao ni kwamba barabara iendayo katika zahanati ya kijiji, inaweza kuwa chanzo cha kifo cha kwanza cha mjamzito au mtoto mchanga, iwapo haitarekebishwa haraka.

“Tunapata taabu sana wakati wa kumsafirisha mjamzito kwenda hospitali ya wilaya,” anasema mwanakijiji aitwaye Lucas Manyosa.

“Barabara ni mbovu. Hatuwezi tena kusubiri Serikali kuu.’’

Mkazi mwingine, Mariam Mwakitalima, anasema: “Hatuna historia ya kifo cha namna hiyo kwa miaka mingi. Kwanini tusubiri hadi kitokee?”.

Mwenyekiti wa kijiji, Charles Mtambalike anasema wanakijiji wameomba wenye magari ya shambani (power tillers), na mengine makubwa wajitolee kwa ajili ya kurekebisha barabara hiyo na wamekubali.

“Wananchi wako tayari na tumeshikamana. Barabara hii ni muhimu kwa afya zetu na uchumi wetu,’’ anasema Mtambalike.

“Ubovu mkubwa uko kilometa 5 kutoka zahanati hadi Barabara ya Mlangali. Hii ni kwa sababu ya nvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni. Kipande hiki cha barabara kinatupa usumbufu mkubwa. Muda unaotumiwa hapo ni mwingi.”

Huku kazi ikiendelea, nakutana na mganga mfawidhi wa zahanati ya kijiji, Wilson Chotamganga, mwenye umri wa miaka 60. Ananiambia kwamba yuko katika mchakato wa kustaafu baada ya kuhudumu kwa takriban miaka 24.

Lakini kumbukumbu ya kusikitisha haijafutika kichwani mwake, ni ya makaburi—madogo kwa makubwa—aliyokutana nayo wakati akianza kazi kijiji hapo mwaka 1993.

“Nilifadhahishwa sana na makaburi. Kwa kiasi kikubwa, kila kaburi lilimaanisha upotevu wa maisha ya mama au mtoto. Nilikutana na makaburi mapya na ya zamani,’’ anasema Chotamganga.

“Hakukuwa na takwimu sahihi. Tuliweza kuhesabu kifo kimoja baada ya kingine hadi kufikia vifo vitano kwa mwaka, watoto hadi 30. Watu walikuwa wakiomboleza na kusononeka muda mrefu sana mama akifa.”

Alisema hayo huku akionyesha tabasamu kwa mbali, labda akishindwa kuficha hisia zake kutokana mafanikio waliyoyapata baadaye kijijini hapo.

“Mbaya zaidi, mwanamke mjamzito alikuwa akifariki na mtoto wake tumboni, watu walikuwa wakisema, hiyo si riziki. Kwangu mimi hii ilikuwa ni ishara ya kukata tamaa. Kwa miaka zaidi ya minne, suluhu haikupatikana, hadi mwaka 1997 tuliposema sasa basi,” anasema mganga huyo.

“Katika sayansi niliyoisoma, ujauzito si ugonjwa. Sasa swali lilikuwa, je, kwanini mjamzito afe? Nilizunguka kijiji kizima, nikitafuta sababu za vifo hivyo, zikabainika. Nikawatangazia watumishi wa zahanati hii, kwamba tutafute suluhisho la hivi vifo.’’

Baada ya dhiki, sasa faraja

Mwaka 1998, mkakati wa kutokomeza vifo ukaanza. Ni baada ya Chotamganga kutambua kuwa watumishi wa zahanati peke yao wasingeweza kuzuia vifo hivyo.

“Nikawambia hebu tuhusishe jamii. Tukaunda kamati tukilenga kuwa na uongozi maalumu wa watu watano ili kutokomeza vifo hivyo katika kijiji hiki na vitongoji vya Ukwama na Mtamba,” anasema.

“Katika kamati hiyo, mmoja alikuwa mwenyekiti wa uzazi na mtoto, katibu wake, pamoja na mtunza fedha. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha zile sheria ndogondogo za halmashauri zinafuatwa. Kwamba, mama asipohudhuria kliniki au kutopeleka mtoto kliniki achukuliwe hatua gani.’’

Kila kitongoji kiliweka mikakati ya kuzuia akina mama kujifungulia nyumbani na kila mwanaume na mwenzi wake wanahudhuria kliniki kuanzia ujauzito hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka mitano. Kwa mujibu wa taarifa za kijijini hapo, familia isiyotekeleza utaratibu huo inatozwa faini hadi Sh50, 000.

Hadi hivi sasa, kamati hiyo imefikia wajumbe 36, wanaojiita “makomando”.

Mmoja wa wanakamati, Josefina Sakarani, 50, ameishi kijijini hapo miaka yake yote.

“Sisi tunaitwa makomando kwa sababu kazi yetu ililenga kutanganza na kutekeleza vita dhidi ya vifo vya wajawazito na watoto,’’ anasema Sakarani.

“Siku za nyuma, akina mama wengi walifariki. Kwanza tulikuwa hatutilii maanani chanjo. Ukiwa na mimba, ukimwambia mume wako twende zahanati kupata ushauri, mume alikuwa akibisha. Tulikuwa tunajifungulia nyumbani.

“Wanawake walichokuwa wanajua ni kusukuma mtoto tu wakati wa kujifungua ukifika. Haijalishi amekaa vizuri au amekaa vibaya kwenye uzazi, wao ilikuwa ni kusuma tu. Kwa namna hii, wengi wamepoteza maisha.’’

Katibu ya afya wa Kijiji cha Uturo, Mariam Kipangule anasema kila mjamzito hufuatiliwa kwa karibu na makomando.

“Na mjamzito yeyote akigundulika na kidokezo cha hatari, zahanati inafanya uamuzi wa kutatua tatizo kama inawezekana au mama huyo hupewa rufaa mapema kwenda hospitali ya wilaya ili kuzuia matatizo makubwa ya uzazi,” anasema.

“Tunaelimisha jamii kila siku kuhusu umuhimu wa kupima. Tangu tuanze mkakati huu mwaka 1998, hatuna kifo cha mjamzito. Manesi wanafanya kazi kwa ukaribu sana na kamati zetu za afya.”

Kwa mujibu wa viongozi wa kijiji, wananchi wako kwenye mchakato wa kujenga wodi ya wazazi inayotegemewa kugharimu Sh300milioni. Tayari wananchi wamechanga fedha kwa ajili ya kujenga msingi. Hivi sasa akina mama wanajifugulia katika chumba ambacho hakitoshelezi mahitaji.

Lakini pia, zahanati ya Uturo inakabiliana na changamoto kama zahanati nyingine ya kawaida.

“Tunahitaji gari la wagonjwa (ambulance). Tukiwa katika dharura huwa tunaita ambulance kutoka wilayani, zaidi ya kilometa 100. Kama limeenda kumfuata mgonjwa mahali pengine, ndipo sisi hulazimika kutafuta magari ya watu binafsi kwa gharama kubwa,’’ anasema bwana Chotamganga.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwanamke mmoja hufariki kila baada ya saa moja wakati wa kujifungua. Hivyo, wanawake 24 wanafariki kwa siku, na 720 kwa mwezi. Kila mwaka, takribani wanawake 8,600. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za wadau na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Cuhas-Bugando), Dismas Matovelo, anasema nguvu ya jamii ikitumika vizuri, inaweka kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kutokomeza vifo hivyo.

“Kwa muda mrefu, jamii zimekuwa zikitegema Serikali na wafadhili katika huduma za mama na mtoto, Lakini mchango wa jamii zenyewe unahitajika kwa kiasi kikubwa,’’ anasema Dk Matovelo.

Hivi karibuni, katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya kuiga mfano wa kijiji cha Uturo katika jitihada za kupambana na vifo vya wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano.

“Kijiji hiki walijitathimini nakuamua kutafiti na kutatua changamoto zao,’’ alisema jijiji Dar es Salaam, alipoulizwa na mwandishi wa makala haya kuhusu Serikali inavyo ihusisha jamii katika kupambana na vifo vya wakawazito na watoto vitokanavyo na uzazi usio salama.

Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Demografia na Afya (TDHS) ya mwaka 2016, vifo vya wajawazito vimeongezeka kutoka 432 hadi 556 kati ya vizazi hai 100,000.

-->