Makula ashangaa kocha kumzushia kuwa mgonjwa

Muktasari:

  • Mwanariadha huyo alisema amesikitishwa na taarifa za kocha mkuu wa timu hiyo, Zacharia Barie kueleza kuwa ameenguliwa kwa sababu ni mgonjwa na nafasi yake kuchukuliwa na Stephano Huche ambaye aliwekwa kama mwanariadha wa akiba.

Arusha. Mwanariadha Said Makula amesikitishwa baada ya kuenguliwa kwenye orodha ya wanariadha watakaokwenda kushiriki mashindano ya Riadha ya Dunia mwezi ujao nchini Uingereza, bila kuelezwa sababu za msingi.

Mwanariadha huyo alisema amesikitishwa na taarifa za kocha mkuu wa timu hiyo, Zacharia Barie kueleza kuwa ameenguliwa kwa sababu ni mgonjwa na nafasi yake kuchukuliwa na Stephano Huche ambaye aliwekwa kama mwanariadha wa akiba.

Alisema, “Tangu nianze mazoezi kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita sijawahi kumwona kocha huyo zaidi ya mwishoni mwa wiki iliyopita, kwani mara nyingi nilikuwa chini ya kocha msaidizi Francis John.”

“Kama anasema mimi naumwa alinipima lini akagundua ugonjwa wangu? Au daktari yupi aliyempa ripoti ya ugonjwa wangu kwa maana kambini hakuna daktari sasa hizo taarifa ya mimi kuwa naumwa alizipata wapi,” alihoji Makula.