Jengo la Yanga ilibidi liuzwe leo

Muktasari:

  • Mkurungezi wa Msolopa Investment Company, Ibrahim Msolopa ameiomba mahakama ya Ilala iwapangie tarehe nyingine watakayofanya mnada wa kuuza jengo la Yanga inayodaiwa deni la Sh. 360 milioni na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Dar es Salaam. Jengo la klabu ya Yanga lililopo mtaa wa Jangwani na Twiga lilipaswa kuuzwa leo Alhamisi badala ya Jumamosi Agosti 19 kama ilivyoonyeshwa katika tangazo lililochapishwa kwenye vyombo vya habari.

Mkurungezi wa Msolopa Investment Company, Ibrahim Msolopa ameiomba mahakama ya Ilala iwapangie tarehe nyingine watakayofanya mnada wa kuuza jengo la Yanga inayodaiwa deni la Sh. 360 milioni na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Msolopa ni dalali wa mahakama amesema, maombi hayo ni baada ya kutokea makosa ya kiufundi katika tangazo lililochapishwa leo Alhamisi kwenye gazeti moja la serikali.

Alisema, tarehe iliyotangazwa ya Agosti 19, siyo ile iliyoamriwa na mahakama, kwa usahihi jengo hilo lililopo maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam, lilitakiwa kupigwa mnada leo Agosti 17.

MCL Digital, iliwatafuta viongozi wa Yanga, katibu mkuu, Charles Mkwasa na Ofisa Habari, Dismas Ten, simu ziliita bila mafanikio.

Timu ya Yanga kwa sasa ipo kambini Pemba ikijindaa na mchezo wake waNgao ya Jamii dhidi ya Simba utakaofanyika Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.