‘Stars ya Simba, Yanga haitufikishi kokote’

Muktasari:

Ni kauli, ushauri wa wadau wa soka kwa makocha

Dar es Salaam. Uteuzi wa wachezaji kwenye kikosi cha Taifa umekosolewa na wadau kwa kuegemea zaidi kwenye klabu za Simba na Yanga kuliko uwezo wa wachezaji wa klabu ndogo.

Ukosoaji huo umefanywa na wadau mbalimbali wa michezo wakieleza kushangazwa na jinsi makocha wa Taifa Stars wanavyowaita wachezaji wanaojiunga na Simba na Yanga.

Kwa nyakati tofauti, wadau hao walidai kuwa licha ya nchi kujaliwa kuwa na wachezaji wengi wazuri wenye vipaji katika klabu mbalimbali kubwa na ndogo wanaofaa kuitwa Stars bila kulazimika kuchezea klabu hizo kongwe, jambo hilo halifanyiki.

Baadhi ya wachezaji walioitwa Stars baada ya kutua Simba au Yanga katika siku za karibuni ni; Juma Mahadhi wa Yanga aliyetokea Coastal Union, Jamal Mnyate wa Simba (alitokea Mwadui), Andrew Vicent ‘Dante’ wa Yanga (alitoka Mtibwa).

Wengine ni, Muzamir Yassin(Simba) aliyekuwa Mtibwa Sugar, Deus Kaseke wa Yanga aliyetokea Mbeya City na Malimi Busungu, pia wa Yanga zamani akiichezea Mgambo JKT.

 

Kilio cha wadau

Kocha Adolph Rishard alisema tatizo ni makocha wa Stars kutozunguka nchini kuangalia mechi nyingi ili kupata wachezaji bora na badala yake huegemea zaidi Simba, Yanga na kidogo Azam.

“Ujue tatizo ni makocha, wanaziona klabu za Dar es Salaam, hapo ndipo huwaona wachezaji, tofauti na wale wa timu ndogo.

“Kwa mfano, wachezaji wa klabu za mikoani huonekana wanapocheza na Yanga au Simba, akishaondoka haonekani tena, hivyo kocha atamchaguaje bila kumuona akicheza mara nyingi ili kujiridhisha na uwezo wake.

“Ni wajibu wa makocha wa Stars kuzunguka nchini mara nyingi ili kuangalia viwango vya wachezaji, vipaji havipo Simba na Yanga, kuna wachezaji wengi wenye vipaji kwenye timu nyingine ndogo wafuatiliwe,” alisema.

Aliongeza: “Zamani, Stars ilichaguliwa kwenye mashindano ya Kombe la Taifa, yaani hadi mchezaji aichezee Stars lazima atoke mbali, wilayani, mkoa hadi Kombe la Taifa, hivyo ilikuwa lazima kuwa na kiwango kizuri.

“Siku hizi, mchezaji anaonekana kwenye ligi, hakuna mashindano mengine ya kuangalia uwezo na ubora wake, ndiyo maana kila mara wataangaliwa zaidi wa Simba, Yanga kwa kuwa wanaonekana mara nyingi.“

Kocha wa zamani wa Stars, Mshindo Msolla alisema tatizo kubwa linalowasumbua makocha wegi siku hizo wakiwa Stars ni kuamini kuwa wachezaji wazuri wanaotakiwa kuichezea timu hiyo lazima watoke Simba na Yanga.

“Uteuzi wa timu ya Taifa unategemea na kocha aliyepo, lakini makocha wengi wa timu yetu wanaamini kuwa ili uwe na kiwango cha kuchezea timu hiyo lazima utoke Yanga au Simba. Kama tutakwenda na dhana hiyo hakika hatutafika kokote.

“Wakati nafundisha timu hiyo mwaka 2002 nilifanya mabadiliko makubwa,nilichagua wachezaji wengi kutoka mikoani kina Danny Mrwanda, Amri Kiemba na wengineo na watu wakanishangaa wakihoji ni timu ile.

“Angalia, wachezaji kama vile, Kichuya, Muzamiru, Kaseke waling’ara na timu zao lakini hakuna aliyekuwa akiwaona na walipojiunga na Simba na Yanga wakaitwa Stars.

“Wapo wachezaji wengi mikoani, ila hakuna mtu wa kuwashika mkono, siyo lazima mchezaji ili awe mzuri hadi awe Dar es Salaam, lazima tubadilike,” alisema Msolla.

Ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alieleza kushangazwa namchezaji kuitwa Stars hadi acheze Yanga au Simba.

“Sijui ni uvivu wa makocha wetu au vipi, sasa tuna kocha mzawa (Charles Mkwasa) anawajua wachezaji wengi na anaweza kuzunguka mikoa mingi kusaka wachezaji, lakini bado wanaitwa wachezaji wengi wa Simba na Yanga.

“Mchezaji akiwa timu ndogo haitwi, akishajiunga na Simba na Yanga anaitwa haraka timu ya Taifa, lazima ifike mahali achaguliwe mchezaji kwa uwezo na siyo jina la timu. Huo ni udhaifu kwani kuna wachezaji wazuri wengi wako timu ndogo, lakini hawaonekani, “alisema Bwire.

Kocha na mchambuzi wa masuala ya soka, Joseph Kanakamfumu alisema siyo sahihi kung’ang’ania wachezaji wa Simba na Yanga, lakini makocha wengi wanaamini kuw klabu hizo zinasajili wachezaji bora na ndiyo maana wengi wanaitwa Stars.

“Ujue Simba na Yanga zinasajili wachezaji bora kutoka klabu ndogo na hiyo inampa urahisi kocha wa Stars kufanya uteuzi wake na wakati mwingine hizo timu husajili wachezaji baada ya kuwaona wameitwa Stars.”

Ofisa habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema alidhani kocha mzawa angeleta mabadiliko, hasa katika uteuzi wa Stars, lakini anashangaa kuona mambo yaleyale ya wachezaji wengi wa Simba na Yanga.

“Mwanzoni nilijua makocha wa kigeni ndiyo tatizo, lakini sasa tuna kocha mzawa, nilijua angeleta mabadiliko, kuzunguka sehemu mbalimbali za nchi kusaka wachezaji, lakini naye ameegemea Simba na Yanga.

“Sisi (Mtibwa) tulikuwa na wachezaji wengi wazuri, lakini hawaitwi Stars, lakini walipojiunga na Yanga na Simba na kucheza mechi moja wameitwa, nawashangaa makocha, sijui tatizo ni nini, kwa nini wanang’ang’ania klabu kubwa wakati wachezaji wengi wazuri wapo,” alisema.

 

Mkwasa ajitetea

Kocha Mkwasa ambaye juzi aliita kikosi cha Stars kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Nigeria alisema anamuita mchezaji ambaye yuko katika kiwango kwa wakati huo.

“Siangalii timu, bali natazama kiwango cha mchezaji. Ukiangalia kwenye kikosi cha sasa wapo wachezaji kutoka timu nyingine tofauti na Simba na Yanga,” alisema Mkwasa.