Kilomoni aondolewa Baraza la Wadhamini Simba, Kapuya apitishwa

Muktasari:

  • Kaimu rais wa klabu hiyo Salim Abdallah alisema kuwa baada ya Kamati ya Utendaji kukaa na kujadili suala hilo, wamefikia maamuzi ya kumtoa katika Baraza la Wadhamini Mzee Kilomoni baada ya kufungua kesi mbili mfululizo.

MKUTANO Mkuu wa klabu ya Simba, kupitia kamati yake ya Utendaji umeamuru kumtoa katika Baraza la Udhamini, Mzee Hamis Kilomoni baada ya kufungua kesi mahakamani ikiwa ni kinyume na katiba ya klabu hiyo. 

Kaimu rais wa klabu hiyo Salim Abdallah alisema kuwa baada ya Kamati ya Utendaji kukaa na kujadili suala hilo, wamefikia maamuzi ya kumtoa katika Baraza la Wadhamini Mzee Kilomoni baada ya kufungua kesi mbili mfululizo. 

"Kamati imefikia hatua hii baada ya kuona kuwa Mzee wetu anakiuka miiko, hivyo tumeona kuwa tunamtoa na nafasi yake inachukuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mguhi, huyu ni mtu sahihi kwetu,"alisema. 

Wakati huohuo kamati ya utendaji imepitisha jina la Juma Kapuya kuwa mmoja wa wadhamini katika Baraza la Wadhamini, akichukua nafasi ya Ally Sykes ambaye ameshatangulia mbele za hali. 

Kapuya alisema kuwa anafurahia kuingia katika baraza hilo, huku akiwashukuru viongozi wa kamati ya Utendaji Kwa kupendekeza jina lake katika baraza la wadhamini wa klabu hiyo ya Simba. 

"Nawashukuru viongozi kwa kupendekeza jina langu, nawashukuru wanachama kwa kupitisha jina langu. Simba ni wanachama na Simba ni Katiba, hakuna mwanachama wala kiongozi aliye juu ya katiba, Simba ni klabu ya mpira, "alisema. 

Pia, kamati ya utendaji imemsimamisha uanachama Mzee Kilomoni na itamuandikia barua ya kumsimamisha, huku wakisubria kujitetea kwake na kufuta kesi mahakamani na asipofanya hivyo atakuwa amejitoa katika uanachama.