Yanga, Simba zasaka kisasi nusu fainali kesho

mashabiki wa Simba na Yanga

Muktasari:

Kamati ya maandalizi ya mashindano hayo ilieleza jana kuwa mchezo huo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Mapinduzi utatanguliwa na ule wa Azam, mshindi wa kwanza Kundi B dhidi ya mshindi wa pili Kundi A aliyekuwa hajajulikana  jana kati ya Jang’ombe Boys, yenye pointi sita sawa na ndugu zao, Taifa Jang’ombe waliokuwa wakicheza usiku na Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) iliyokuwa na pointi nne, ambayo ikishinda ingefuzu kwa pointi saba.

Zanzibar. Baada ya sare ya bao 1-1, Oktoba Mosi mwaka jana kwenye mzunguko wa Kwanza wa Ligi Kuu iliyotawaliwa na matukio lukuki yakiwamo; bao la mkono la Amissi Tambwe, kadi nyekundu ya utata ya  Jonas Mkude, vurugu za mashabiki waliovunja viti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na bao la kona ya moja kwa moja la Shiza Kichuya akimtungua kipa Ally Mustapha Barthez, aliyegeuka mtazamaji hadi leo, Yanga na Simba kesho usiku zitahamishia upinzani wao kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa.

Kamati ya maandalizi ya mashindano hayo ilieleza jana kuwa mchezo huo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Mapinduzi utatanguliwa na ule wa Azam, mshindi wa kwanza Kundi B dhidi ya mshindi wa pili Kundi A aliyekuwa hajajulikana  jana kati ya Jang’ombe Boys, yenye pointi sita sawa na ndugu zao, Taifa Jang’ombe waliokuwa wakicheza usiku na Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) iliyokuwa na pointi nne, ambayo ikishinda ingefuzu kwa pointi saba.

Mchezo huo wa Jumanne unaweza kuitwa wa kisasi au fainali iliyokuja mapema baada ya maajabu ya Azam FC iliyoizidi kete Yanga Jumamosi usiku na kuibugiza mabao 4-0 na jana Simba ilimaliza kazi  Kundi A ikiwa kinara baada ya kuilaza Jang’ombe Boys kwa mabao 2-0 ya Laudit Mavugo, moja kila kipindi. 

Zilifuzu  kwenye mazingira tofauti ya ubora

Jumamosi, Yanga iliyoanza kishindo na vipigo dhidi ya wenyeji Jamhuri ya Pemba, mabao 6-0 na Zimamooto mabao 2-0, ilikosa mbinu za kurudi mchezoni baada ya kufungwa na Azam bao la mapema kipindi cha kwanza, ilijikuta ikilazimika kukimbiza upepo kwa muda mwingi wa mchezo na kuwaacha vijana wa Azam chini ya kocha wa muda, Idd Nassor ‘Cheche’ wakichanua kila mahali uwanjani.

Watani zao, Simba wamekuwa na ukame wa mabao, waliibuka na na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KVZ na 2-1 dhidi ya Taifa Jang’ombe, sare ya 0-0 dhidi ya URA,  kuituliza Jang’ombe Boys.