Polisi yawagomea makomandoo Simba, Yanga

Muktasari:

Mwanzoni makomandoo hao walianza kulindana wenyewe nje ya uwanja huo ili kuhakikisha kuwa hakuna upande utakaoingia ndani na kufanya vitendo vya kishirikina.

Jeshi la Polisi limewakomoa makomandoo wa Simba na Yanga baada ya kuwalaza nje ya Uwanja wa Taifa kwa siku mbili mfululizo kabla ya pambano la timu hiyo la leo jioni.

Ulinzi mkali uliowekwa na jeshi hilo tangu mwanzoni mwa wiki hii, uliwafanya makomandoo wa timu hizo kuambulia patupu baada ya kushindwa kuingia uwanjani na kufanya vitendo vya kishirikina kama ilivyozoeleka.

Mwanzoni makomandoo hao walianza kulindana wenyewe nje ya uwanja huo ili kuhakikisha kuwa hakuna upande utakaoingia ndani na kufanya vitendo vya kishirikina.

Idadi kubwa ya makomandoo wa Yanga ambao walikuwepo uwanjani hapo, iliwafanya waweze kuwadhibiti wenzao wa Simba na kuamini kuwa wangeweza kuingia uwanjani kirahisi ili kukamilisha mipango yao.

Hata hivyo, nao walijikuta wakidhibitiwa ipasavyo na jeshi la Polisi ambalo limeonekana kujipanga vilivyo hivyo kushindwa kuingia ndani ya uwanja huo hadi asubuhi ya leo.

"Kama unavyoona wewe mwenyewe jinsi tulivyojipanga kuhakikisha hakuna anayeingia humu hadi kesho (leo) ambapo taratibu za kawaida za mchezo zitakapoendelea.

"Safari hii hatutokuwa tayari kuruhusu mambo ya kishirikina hivyo hao jamaa wa Simba na Yanga waendelee kukaa hapo hapo nje hadi kesho (leo asubuhi)," alisema mmoja wa maofisa wa Polisi aliyekuwepo uwanjani hapo jana usiku.

Udhibiti huo wa jeshi la Polisi ulionekana kuwaleta makomandoo hao ambao walijitawanya mafungu mafungu nje ya uwanja huo huku wakiwa na vitu mbalimbali vinavyosadikiwa kuwa ni dawa ambazo walipanga kwenda kuziweka uwanjani hapo.

"Hali ni tete na Polisi wanaonekana kukomaa, lakini tutahakikisha tunatumia mbinu yoyote kuhakikisha dawa hizi tunakwenda kuziweka," alitamba komandoo mmoja wa Yanga