Serengeti Boy ni zaidi ya timu

Muktasari:

Serengeti Boys ipo katika maandalizi ya fainali za vijana chini ya miaka 17 zitakazoanza Mei 24 hadi Juni 4 ambako timu nne zinazofuzu kwa nusu fainali zinakata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia la Fifa.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Serengeti Boys, Yohana Mkomola amesema sasa wamekuwa zaidi ya timu kwa kuwa wamezoeana kama watoto wa familia moja jambo litakalowasaidia kufanya vizuri katika mashindano ya Gabon.  
Serengeti Boys ipo katika maandalizi ya fainali za vijana chini ya miaka 17 zitakazoanza Mei 24 hadi Juni 4 ambako timu nne zinazofuzu kwa nusu fainali zinakata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia la Fifa.
Mkomola alisema maandalizi yetu yanakwenda vizuri kila siku, tuko pamoja kwa muda sasa kila mmoja amekuwa akijitahidi kusikiliza mafunzo kwa makini tunayofundishwa na walimu wetu.
"Tumekuwa kama familia moja nitakuwa sikosei kama nikisema kikosi chetu kipo kwenye hatua nzuri ya kimaandalizi ambayo ni muhimu kwakuwa kama tunaishi na kucheza kama familia itatusaidia kufanya vizuri katika fainali hizi," alisema Mkomola.
Mkomola ni mchezaji anayelelewa Azam Academy na tayari amefuzu majaribio yake ya kucheza soka la kulipwa nchini Tunisia katika klabu ya Etoile du Sahel.
Mshambuliaji huyo atajiunga na miamba hiyo ya Tunisia baada ya kumalizika kwa fainali za Gabon.