Thursday, April 20, 2017

 

By Fredrick Nwaka, Mwananchi

Prisons yajichimbi Dar ikisubiri Yanga
Fredrick Nwaka, Mwananchi
Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Prisons, Abdallah Mohammed amesema timu yake ilifika mapema Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa mwisho wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.
“Yanga ni timu kubwa na imetoka kushiriki mashindano ya kimataifa lakini hiyo haitupi hofu, wachezaji wangu wana ari ya mchezo na tumenuwia kushinda,” alisema kocha huyo.
Beki wa kulia wa timu hiyo, Salum Kimenya alitamba kuwa hawatakubali kufungwa na Yanga baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu.
Prisons itaingia katika mchezo huo ikitokea Mwanza ambako ilifungwa bao 1-0 na Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana.
Wakati huohuo Yanga inaingia kambini leo, kuanza maandalizi ya mchezo huo.
Tayari Azam, Simba na Mbao zimefuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo ambayo bingwa wake kuchukua Sh 50 milioni, pamoja na kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

-->