Thursday, April 20, 2017

 

By Charles Abel, Mwananchi

Samatta asaka nauli usiku huu

Charles Abel, Mwananchi

Dar es Salaam. Dakika 90 za mechi ya Europa Ligi  leo usiku dhidi ya Celta Vigo zinaweza kuwa hitimisho kwa ndoto ya muda mrefu ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayechezea RCK Genk ya Ubelgiji kwenye mashindano hayo.

Genk itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kuikaribisha Celta Vigo huku timu hiyo ya Samatta inahitaji ushindi wa bao 1-0 tu ili kufuzu hatua ya
nusu fainali ya mashindano hayo.
Kama Genk watapata ushindi na kufanikiwa kufuzu nusu fainali, huenda wakakutana na Manchester United, klabu ambayo Samatta mara kwa mara amekuwa akitamani kukutana nayo na hasa kucheza kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Katika mahojiano yake kadhaa aliyofanya siku za nyuma, Samatta aliwahi kukiri kutamani kupangwa na kukutana na Manchester United, akiamini kuwa hiyo itakuwa nafasi kwake kucheza kwenye Uwanja wa Old Trafford na kutimiza ndoto zake.

"Nilikuwa naomba ratiba ratiba itokee, tunakutana na Manchester United kwa sababu ndoto yangu ya
kukanyaga Old Trafford itakuwa imetimia.

Nina ndoto ya kukanyaga Old Trafford kwani
ukiachana na mambo mengine, huenda hiyo ikawa ndio
fursa au njia kwangu, lakini hayo yatakuja baadaye
kwenye mchezo ila nitajua naenda kukanyaga pale ambako nimekuwa nikiota," aliwahi kunukuliwa Samatta.

Manchester United iko kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua hiyo ya nusu fainali, kutokana na kuhitaji ushindi wa aina yoyote kwenye mchezo wa leo itakapokuwa nyumbani kuwakaribisha Anderlecht ya Ubelgiji waliyotoka nayo sare ya bao 1-1 ugenini.

Pengine ndoto hiyo inaweza kumpa hamasa zaidi Samatta kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo kama ambavyo amekuwa akifanya katika siku za hivi karibuni ambapo amekuwa moto wa kuotea mbali ndani ya kikosi cha Genk.

Ndani ya msimu huu pekee, Samatta ameifungia Genk
mabao mabao 12 katika mechi 38 alizoichezea kwenye
mashindano mbalimbali msimu huu huku pia akipiga pasi tano zilizozaa mabao katika mechi za timu hiyo kwenye mashindano tofauti ambayo wameshiriki
msimu huu.

Kutokana na Samatta kuanza kuzitoa udenda baadhi
ya timu barani humo, kuna uwezekano mkubwa mechi
ya leo kukawepo na kundi la maskauti wa soka kwa lengo la kumtazama mshambuliaji huyo kama ilivyotokea kwenye mchezo uliopita ambapo Fernebahce ya Uturuki ilimtuma meneja wake Hasan Çetinkaya kwa lengo la kumtazama Samatta na mchezaji wa Celta Vigo, Theo Bongonda.

Mbali na Fernebahce, tayari kulikuwepo na taarifa za Samatta kuzivutia timu za Wolsfburg, Hamburger SV na Borussia Moenchengladbach zinazoshiriki ligi
kuu ya England.

Mbali na mechi hizo zinazohusu Genk na Manchester
United, mechi nyingine za leo zitazikutanisha Schalke 04 dhidi ya Ajax wakati Besiktas wataialika Olympique Lyon.

-->