AFC Arusha yasaka nyota wa kusajili

Muktasari:

Mwenyekiti wa AFC, Charles Mnyalu alisema tayari wachezaji hao wameanza mazoezi chini ya kocha Juma Masoud na kufungua milango kwa wachezaji wengine kujitokeza kutafuta nafasi ya kusajiliwa.

Arusha. Uongozi wa AFC Arusha umewaita wachezaji 40 kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi daraja la pili (SDL), pamoja na kuweka mikakati ya kucheza michezo ya kirafiki ndani na nje ya mkoa.

Mwenyekiti wa AFC, Charles Mnyalu alisema tayari wachezaji hao wameanza mazoezi chini ya kocha Juma Masoud na kufungua milango kwa wachezaji wengine kujitokeza kutafuta nafasi ya kusajiliwa.

“Hata kama watafiki wachezaji 60 hilo siyo tatizo, maana dirisha la usajili litakapofunguliwa kocha pamoja na benchi la ufundi wataangalia ni mchezaji yupi anayefaa kusajiliwa.”

“Hii ni timu ya wananchi na imeyumba kwa muda mrefu, lakini kwa sasa imetosha hivyo wanachama wanatakiwa tuungane na tusahau yote yaliyotokea nyuma bali tushirikiane katika kulisukuma gurudumu hili,” alisema Mnyalu.

Mnyalu alisema malengo yao ni kutafuta mechi za kirafiki na klabu kubwa nchini ikiwamo Simba, Yanga na Azam, ili kurudisha hamasa kwa mashabiki wa mkoa wa Arusha akiamini kuwa atafanikiwa kurudisha mshikamano uliopotea.