Agenda ya MO kufunika mkutano wa Simba leo

Mohammed Dewji

Muktasari:

Licha ya kuwapo na agenda mbalimbali ikiwamo ya usajili, mapato na matumizi ya klabu na maendeleo ya klabu, suala kubwa linalotarajia kuibua mvutano ni uwekezaji wa Mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘MO’ aliyepanga kuwekeza Sh20bilioni katika klabu hiyo.

Dar es Salaam. Wanachama wa klabu ya Simba wanakutana katika mkutano mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam leo.

Licha ya kuwapo na agenda mbalimbali ikiwamo ya usajili, mapato na matumizi ya klabu na maendeleo ya klabu, suala kubwa linalotarajia kuibua mvutano ni uwekezaji wa Mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘MO’ aliyepanga kuwekeza Sh20bilioni katika klabu hiyo.

Uzoefu wa klabu za Simba na Yanga, viongozi hubanwa hasa eneo la mapato na matumizi ya klabu, lakini safari hii linaonekana kutokuwa na nguvu zaidi ya suala la uwekezaji wa MO klabuni hapo.

Suala hilo ndilo linalofanya wanachama na mashabiki wa Simba kuzozana kila mahali huku kila mmoja akitoa hoja kwa kadri ya upeo wake kuhusu uwekezaji huo.

Baadhi ya wanachama wa Simba walisema wanatarajia kila hoja itakayowasilishwa katika mkutano wa leo itapewa uzito unaostahili ili kuhakikisha Simba inakuwa na umoja na kupata mafanikio.