Aguero hatarini kuikosa Man United

Muktasari:

Tukio hilo lilinaswa katika picha za video na zinaweza kutumika kumfungia mchezaji huyo na kuukosa mchezo wa Septemba 10 kama mwamuzi Andre Marriner atathibitisha kwamba hakuliona tukio hilo.

London, England. Sergio Aguero anaweza kukosa mchezo wao ujao wa mahasimu wa Jiji la Manchester baada ya kuonekana akimpiga kiwiko Winston Reid.

Tukio hilo lilinaswa katika picha za video na zinaweza kutumika kumfungia mchezaji huyo na kuukosa mchezo wa Septemba 10 kama mwamuzi Andre Marriner atathibitisha kwamba hakuliona tukio hilo.

Aguero anaweza kufungiwa kwa mechi tatu na Chama cha Soka England (FA) kama mwamuzi Marriner, ambaye alikuwa karibu kwa umbali wa mita tano kutoka eneo la tukio wakati Manchester City ikishinda mabao 3-1 dhidi ya West Ham United, akithibitisha kuwa hakuona tukio hilo.

FA inajiandaa kumchukulia hatua mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina kama Marriner akithibitisha, jambo ambalo linaweza kumkosesha mchezo ujao dhidi ya Manchester United Septemba 10.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola alisema: “Mimi ni mgeni hapa, hivyo sijajua bado sheria hapa zinasemaje juu ya hilo.

“Sikuona tukio, Hivyo siwezi kutoa maoni katika hilo. Bila shaka hakuna kibaya kitakachotokea. Kama kitatokea tutakubaliana nacho. Tukimkosa, haitajalisha kwani bado tutacheza 11.” Reid alilazimika kutoka uwanjani baada ya kupigwa kiwiko na Nahodha wa West Ham, Mark Noble akisema kuwa mwenzake huyo alishindwa hata kuzungumza ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo.

“Mimi sikuona tukio, nwe mkweli,” alisema kiungo huyo wa West Ham, Noble.

“Sikujua hata nini kilimwangusha. Ninachojua ni kwamba alishindwa kuzungumza vyumbani. Alisema hawezi kwa sababu anapata maumivu makali katika koo.”

Aguero alishahusishwa kwenye tukio la aina hiyo alipomkanyaga David Luiz katika mchezo wa Kombe la FA hatua ya nusu fainali.

Kwa mshangao, Aguero alitoka bila kupata adhabu yoyote kwa tukio hilo, wakati beki huyo wa Brazil akisema hakuwahi kuombwa radhi na Aguero licha ya mshambuliaji huyo kusema alifanya hivyo kupitia mtandao wa Twitter.