Arsenal inakabiliwa na vita mbili, asema Wenger

Muktasari:

Kufungwa katika mechi mbili mfululizo, ikiwamo cha mabao 3-1 dhidi ya Chelsea wiki iliyopita kumeifanya Arsenal kushuka hadi nafasi ya nne.

London, England. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri timu yake inakutana na mtihani wa kumaliza ndani ya timu nne za juu huku ikiwa bado na lengo la kuifukuza Chelsea kileleni.

Kufungwa katika mechi mbili mfululizo, ikiwamo cha mabao 3-1 dhidi ya Chelsea wiki iliyopita kumeifanya Arsenal kushuka hadi nafasi ya nne.

Lakini ipo mbele ya Manchester United inayoshika nafasi ya sita, wakati ikiachwa kwa pointi 12 dhidi ya kikosi cha kocha Antonio Conte.

Wenger alisema kikosi chake kinaingia katika vita ya mapema ya msimu ya kukimbia kumaliza nje ya nafasi nne za juu kwa mara ya kwanza tangu 1995/96.

“Unapokuwa mshindani unatakiwa kuonyesha kweli unapambana,” aliyaambia magazeti ya Uingereza.

“Unapambana kadri uwezavyo na sasa tupo katika vita mbili. Ya kwanza tunapambana kumaliza ndani ya nafasi nne za juu, pia ni kwa sababu tunapambana kuitafuta ilipo Chelsea. Tunatakiwa kukataa kukata tamaa,” alisema.

Wenger anaweza kuirudisha timu mchezoni kama ataifunga Hull City katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu England.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema kikosi chake kinatakiwa kuelekeza akili katika wakati huu aliouita muhimu zaidi katika msimu.