Arsenal kufuta uteja kwa Chelsea

Muktasari:

Vita kali katika mchezo huo wa saa 1:30 jioni itakuwa baina ya mwajiri, Chelsea dhidi ya kipa, Cech kama ilivyo kwa Cesc Fabregas dhidi ya Arsenal.

London, England. Ni miaka sita imepita tangu Arsenal ilipofunga bao kwenye mchezo dhidi ya Chelsea kwenye Ligi Kuu England. Pia, ushindi utategemea washambuliaji wao dhidi ya umahiri wa makipa Petr Cech na Thibaut Courtois.

Vita kali katika mchezo huo wa saa 1:30 jioni itakuwa baina ya mwajiri, Chelsea dhidi ya kipa, Cech kama ilivyo kwa Cesc Fabregas dhidi ya Arsenal.

Ni miaka sita tangu Arsenal ikiwa na; Fabregas, Robin van Persie, Samir Nasri, Gael Clichy na Alex Song kikosini ilipoishinda Chelsea kwenye mechi ya ligi.

Mchezo huo kwenye Uwanja wa Emirates, unazikutanisha timu zenye mifumo tofauti ya kiuchezaji.

Mifumo yao

Kocha Arsene Wenger anatumia 4-2-3-1, dhidi ya mpinzani wake, Antonio Conte na mfumo wake wa 4-3-3.

Timu zao zina pointi 10 kila moja, zinashika nafasi ya nne na tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Vita kali itaonekana kwa mabeki wa Arsenal dhidi ya mbaya wao, Diego Costa ambaye kwa misimu miwili amewatungua. Pia, akiwasababishia kadi nyekundu, Laurent Koscielny na Per Mertesacker ambaye kwa sasa ni majeruhi.

Upande wa pili, Alexis Sanchez anayeng’ara, ana kibarua cha kuiongoza Arsenal kufuta uteja, akisaidiana na; Olivier Giroud, Alex Iwobi au Theo Walcott ili kuwalaza mapema Chelsea.

Arsenal haijafunga bao kwenye mechi sita dhidi ya Chelsea tangu Walcott alipofanya hivyo Januari 2013, kwenye kipigo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Hivyo, huo ni mchezo unaomkutanisha Cesc Fabregas dhidi ya kocha wake wa zamani, Wenger, akiiongoza kwa mara ya kwanza klabu hiyo tangu atimize miaka 20 juzi.

Kwa upande mwingine, Antonio Conte aliyeiongoza timu yake kwa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Liverpool, ana kibarua kigumu cha kumridhisha mwajiri wake, Roman Abramovich.

Fabregas, hajaanza mchezo wa Ligi Kuu msimu huu chini ya Conte, aliiwezesha timu yake kusonga mbele dhidi ya Leicester City Jumatano kwa mabao yake mawili kati ya manne kwenye Kombe la Ligi (EFL).