Azam kumnasa aliyeiua Yanga

Daniel Amoah wa Madeama.

Muktasari:

Akizungumza na gazeti hili mjini Accra, ofisa mtendaji mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema walitaka kuwasajili wachezaji wawili wa  Medeama, lakini walilazimika kumsajili  Atta kwanza

Accra. Baada ya kukamilisha usajili wa kiungo Enock Atta Agyei, klabu ya Azam imerudi tena Ghana na kufanya mazungumzo na nyota mwingine wa Medeama, Daniel Amoah.

Azam ilimalizana na Atta kutoka Medeama mwanzoni mwa wiki kwa kumsajili kwa mkataba wa miaka miwili na anatarajiwa kutua nchini wakati wowote  kujiunga na timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili mjini Accra, ofisa mtendaji mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema walitaka kuwasajili wachezaji wawili wa  Medeama, lakini walilazimika kumsajili  Atta kwanza kutokana na vipengele vya mkataba wake na makubaliano.

Kawemba alisema Atta alikuwa mwishoni  mwa mkataba wake na ilikuwa rahisi kufanya hivyo na kumleta nchini haraka zaidi,  lakini kwa Amoah hilo limekuwa gumu kutokana na sababu za msingi za Medeama.

Mtendaji huyo wa Azam alisema Medeama walishakubali kumtoa Amoah, lakini waliomba aendelee kuitumikia timu hiyo hadi Novemba ili kuwasaidia katika michezo yao migumu iliyobaki ya Ligi Kuu na ya kimataifa.