BRAZIL 2014: Vita ya wachana nyavu

Straika wa Ufaransa Karim Benzema (kushoto) leo atapambana na mwenzake Mjerumani Thomas Mueller wanapokutana kule Estadio de Maracana, Rio de Janeiro usiku huu. PICHA || AFP  

Muktasari:

Ufaransa inaivaa Ujerumani, wakati Brazil watajiuliza mbele ya Colombia katika robo fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia.

Rio de Janeiro, Brazil. Ukizubaa, imekula kwako! Hiki ndicho kinachotarajiwa kutokea leo wakati washambuliaji vinara wa ufungaji watakapoonyeshana ubavu katika mechi za robo fainali ya Kombe la Dunia.

Ni vita baina ya Karim Benzema wa Ufaransa  dhidi ya Thomas Mueller wa Ujerumani, huku Neymar akiiongoza Brazil kuikabili Colombia usiku ikiwa chini ya kinara wao,  James Rodriguez mwenye mabao matano.

Hali hiyo inazifanya mechi zote za leo ziwe kivutio kikubwa huku nyota hao wakitaka kuonyesha nani zaidi.

Tayari, mechi 56 zimeshachezwa hadi sasa na kuleta matokeo ya kushangaza. Mabao 154 yamefungwa ukiwa ni wastani wa mabao 2.75 kwa mechi na kuzifanya fainali hizi za Brazil  kukaribia kuivunja rekodi ya mabao 171 iliyowekwa katika Kombe la Dunia la Ufaransa  mwaka 1998.

Nadharia ya kupatikana mabao mengi kiasi hiki inatokana na kubadilika kwa sheria, mabadiliko ya mbinu, kupungua kwa uwezo wa mabeki ni mambo yaliyoongeza utamu wa fainali hizi za Brazil.

Kocha wa zamani wa Ufaransa, Gerard Houllier anaamini hiyo inatokana na uwezo wa washambuliaji chipukizi waliopo katika fainali hizo.

“Neymar, (Lionel) Messi, Benzema, (Robin) Van Persie, (Arjen) Robben, Rodriguez ni wachezaji wa kiwango cha juu,” alisema Houllier.

Orodha hiyo ya wafumania nyavu wataanza kumalizana leo wakati Ufaransa itakapoivaa Ujerumani kwenye Uwanja wa Maracana, Rio de Janeiro, kabla ya wenyeji Brazil kuikabili Colombia mjini Fortaleza.

Kesho kutashuhudiwa Argentina ikiivaa Ubelgiji ikiwa ni marudio ya nusu fainali ya Kombe la Dunia  mwaka 1986, huku Uholanzi ikiivaa timu ndogo isiyotabirika kutoka Amerika ya Kati, Costa Rica.

Ufaransa kisasi  Ujerumani

Mechi ya Ufaransa na Ujerumani inakumbusha timu hizo zilipokutana kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia 1982, wakati Ujerumani ilipolazimishwa sare 3-3, kabla ya kushinda kwa penalti 5-4.

Mechi hiyo ya mjini Seville iliharibiwa na tukio la kipa wa Ujerumani, Harald Schumacher kumpiga teke la kung- fu mchezaji  wa Ufaransa, Patrick Battiston na kumvunja mbavu, meno matatu na kusababisha kuzirai uwanjani.

Wakati vyombo vya habari vikiuliza kama Ufaransa italipa kisasi kwa tukio hilo, makocha Joachim Loew na Didier Deschamps walisema haiwezi kuwa hivyo kwa sababu wachezaji wote wanaocheza sasa walikuwa hawajazaliwa tukio hilo lilipotokea.

Wakati Benzema akiwa katika kiwango kizuri, Ufaransa inaota kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya nyingine tangu 1998 walipokuwa nyumbani, lakini macho na mawazo yao ni kwa Ujerumani.

“Kila mmoja anaweza kuliota hilo, pamoja na mimi, lakini nina uhakika inawezekana, Ijumaa ndio siku itakayotoa majibu,” alisema   Deschamps.

Kuhusu Mueller, Ujerumani pia inamwangalia kwa ukaribu mpachika mabao wao, nyota wa Bayern Munich ambaye ameshafunga mabao manne hadi sasa.

Lakini hata Mueller amekuwa akimwangalia vizuri mshambuliaji wa Colombia mwenye namba 10 mgongoni, Rodriguez, ambaye anaongoza kwa ufungaji, akiwa na mabao matano.

Kinda huyo mwenye miaka 22 ameonyesha ubora wake katika fainali hizo, hasa alipofunga bao maridadi dhidi ya Uruguay katika hatua ya mtoano 16, na sasa anatolea macho zawadi muhimu nchini Brazil.

Kiwango cha Neymar, mwenye bao moja nyuma ya Rodriguez kinaweza kutoa matumaini ya wenyeji hao wa fainali za mwaka huu.