Bao la ‘usiku’ laibeba Simba

Muktasari:

Licha ya Mbao FC kucheza vizuri na kuwazuia washambuliaji wa Simba kwa muda mwingi, kosa la dakika 86, lilitosha kumpa mwanya kiungo Muzamiru Yassin kufunga bao pekee baada ya kupokea pasi ya kichwa ya Frederick Blagnon aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Laudit Mavugo.

Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu, Simba wameendelea kujikita kileleni baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC kwenye mchezo uliojaa ufundi.

Licha ya Mbao FC kucheza vizuri na kuwazuia washambuliaji wa Simba kwa muda mwingi, kosa la dakika 86, lilitosha kumpa mwanya kiungo Muzamiru Yassin kufunga bao pekee baada ya kupokea pasi ya kichwa ya Frederick Blagnon aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Laudit Mavugo.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 26, nane zaidi ya watani zao na mabingwa watetezi, Yanga iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na pointi 18 huku wakiizidi Azam kwa pointi 13.

Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Mbao, lakini nidhamu ya mchezo ya vijana hao wa Mwanza iliwazuia Simba kupata bao mapema.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ilipata kona saba, lakini safu ya ulinzi ya Mbao iliyoongozwa na kipa Emmanuel Mseja ilikuwa makini kuondosha hatari zote.

Dakika ya 19, na 42, kipa Mseja alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa kichwa wa Mavugo na shuti la Ibrahim Ajibu, mashambulizi ambayo pengine yangeifanya Simba iende mapumziko ikiongoza.

Shambulizi pekee kwa Mbao lilikuwa ni dakika ya 37, lililofanywa na mshambuliaji mkongwe na nahodha wa timu hiyo, Hussein Sued, lakini shuti lake liliokolewa vyema na kipa Vincent Angban na kuwa kona isiyozaa matunda.

Kocha wa Mbao, Etienne Ndayiragije alilazimika kuanza na mfumo wa 4-5-1 kama unaotumiwa na Simba, jambo lililoonekana kuisaidia timu hiyo kipindi cha kwanza.

Vikosi

Simba

Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Muzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya.

Mbao FC: Emmanuel Mseja, Steven Sylvester Mgaya, Steven Kigocha, Asante Kwasi, Robert Magadula, Yusuf Ndikumana, Dickson Ambundo, Salmin Hoza, Hussein Sued, Emmanuel Mvuyekule, Pius Buswita.