Bao langu zuri zaidi ya Mkhitaryan- Giroud

Muktasari:

Giroud alifunga bao zuri dhidi ya Crystal Palace Januari Mosi, akiamsha mguu wake wa kushoto kwa nyuma na kuuinua mpira juu ya kipa Wayne Hennessey katika kona ya mbali ya lango.

London, England. Mshambuliaji wa Arsenal, Olivier Giroud ametania kuwa bao lake alilofunga kwa kisigino kwa mtindo wa ng’e ni bora zaidi ya lile alilofunga Henrikh Mkhitaryan wa Manchester United.

Giroud alifunga bao zuri dhidi ya Crystal Palace Januari Mosi, akiamsha mguu wake wa kushoto kwa nyuma na kuuinua mpira juu ya kipa Wayne Hennessey katika kona ya mbali ya lango.

Mkhitaryan alifunga kwa aina hiyo hiyo dhidi ya Sunderland wiki moja nyuma na kuliita bao la mwezi Desemba.

Hata hivyo, Giroud anaamini kuwa bao lake lilikuwa na utamu wa aina yake kutokana na eneo ambalo mpira ulikwenda.

“Bila shaka walikuwa wananitania, waliniambia bao la Mkhitaryan ni miongini mwa mabao bora!” alisema katika kipindi cha maswali na majibu cha mtandao wa Soccer AM.

“Inashangaza kuona mabao mawili yanayofanana yanafungwa ndani ya wiki moja. Sidhani kama la mwenzangu lilinishawishi kufunga kwa mtindo ule, ilitokea tu.

“Alifunga vizuri pia, lakini nadhani langu lilikuwa bora zaidi! Tuwe wakweli ilikuwa furaha sana ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo, wote tulishangaa kwa kilichotokea,” aliongeza.

Giroud amefunga mabao saba katika Ligi Kuu msimu huu, wakati Arsenal ikikaa katika nafasi ya nne kwenye msimamo, ikiwa nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi nane.