Beki wa zamani Yanga avaa gwanda

Beki Edward Manyama aliyewahi kukipiga katika klabu ya Yanga, ameamua kuachana na maisha ya kiraia na kukimbilia kuvaa gwanda, baada ya kuona maisha ya vilabu vya Bongo hayaeleweki katika kipindi kifupi alichocheza ligi.

Manyama alisema kuwa aliangalia hali halisi jinsi ambavyo ilikuwa baada ya kutoka Yanga na kwenda katika Ligi Daraja la Kwanza na kuona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kubadili uamuzi na kuvaa gwanda.

“Nilianzia maisha nikiwa hapa JKT Ruvu na kabla ya Yanga kunifuata kuna nafasi ziliwahi kutoka lakini sikutilia maanani, kwa sababu tayari vilabu vikubwa vilishaanza kuonyesha nia ya kunihitaji mpaka nikatua Yanga, lakini nimeona bora nivae gwanda kwa sababu huku kuna maisha ya kudumu,” alisema.

Beki huyo ambaye msimu uliopita timu yake ya JKT Ruvu ilishuka daraja alisema kuwa kutokana na uzoefu wao wa Ligi Kuu na wenzake katika timu hiyo anaamini kuwa watapambana Ligi Daraja la Kwanza ili warudi Ligi Kuu.

Manyama alianza kuichezea JKT Ruvu na baadaye akasajiliwa na klabu ya Yanga na kisha akaichezea klabu ya Geita Gold katika Ligi Daraja la Kwanza na msimu uliopita alirudi Ruvu na kushuka nayo Ligi Daraja la Kwanza.