Bocco awabipu Tambwe, Mavugo

John Bocco

Muktasari:

Hadi sasa, Bocco anaongoza kwenye chati  ya wafungaji akiwa amefunga mabao matatu huku mfungaji bora msimu uliopita, Amissi Tambwe akianza ligi bila bao, sawa na Donald Ngoma, wakati Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon wa Simba wakiwa na bao moja kila mmoja.

Dar es Salaam. Mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ ameanza na moto kwenye Ligi Kuu Bara na kuwatimulia vumbi maproo wanaoimbwa kila wakati, lakini mwenyewe amesema anachoangalia ni kuisadia timu kwanza.

Hadi sasa, Bocco anaongoza kwenye chati  ya wafungaji akiwa amefunga mabao matatu huku mfungaji bora msimu uliopita, Amissi Tambwe akianza ligi bila bao, sawa na Donald Ngoma, wakati Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon wa Simba wakiwa na bao moja kila mmoja. Bocco, Tambwe na Ngoma ni miongoni mwa washambuliaji watano walioongoza kwa kufunga mabao msimu uliopita sambamba na Hamis Kiiza na Kipre Tchetche.

Wakati Bocco akitamba, Tambwe na Ngoma bado hawajaanza kuziona nyavu licha ya ushindi wa mabao 3-0 ambao Yanga iliupata dhidi ya African Lyon juzi.

Mabao hayo ya Bocco yamekuwa msaada mkubwa katika kuipeleka Azam kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi nne sawa na Simba ingawa wanabebwa na faida ya kuwa na mabao mengi ya kufunga.

Mavuno ya kupoteza nyota wake muhimu wa kikosi chake cha kwanza msimu uliopita, yanaanza kuonekana sasa kwa Majimaji ambayo imeanza ligi vibaya kwa kushika mkia baada ya kufungwa dhidi ya Prisons kwa bao 1-0 kisha ikapoteza 3-0 mbele ya Azam.

Bocco alisema yeye huwa hataki mbwembwe, mambo yake kimya kimya kwani malengo yake ni kuisaidia Azam kutwaa ubingwa msimu huu na mambo ya ufungaji bora yatafuata.

Bocco anaamini kuwa kwa kikosi walichonacho wana kila sifa za kubeba taji msimu huu licha ya kwamba ligi ina ushindani na changamoto nyingi.

“Tunafurahi tumeshinda mchezo uliopita dhidi ya Majimaji na kuongoza ligi, kinachotakiwa ni kuendelea kujituma ili tushinde mchezo ujao.

“Mechi ijayo tunacheza ugenini na Prisons, ni moja ya mechi ngumu kwani wapinzani wetu ni hatari wanapokuwa kwenye uwanja wao, hivyo lazima tujipange kuwakabili,” alisema Bocco.

Aliongeza: “Malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu na kwa aina ya kikosi tulichonacho naamini tutatimiza hilo, nitajituma kuhakikisha nafunga kila mara ili kuisaidia timu yangu ifanye vizuri na wala siuwazii ufungaji bora.”

Bocco alisema yeye huwa hataki mbwembwe, mambo yake kimya kimya kwani malengo yake ni kuisaidia Azam kutwaa ubingwa msimu huu na mambo ya ufungaji bora yatafuata.