Cioaba:Tuko tayari kwa mbio za ubingwa Ligi Kuu

Muktasari:

  • Azam iliweka kambi ya siku 10 nchini Uganda kujiandaa na ligi hiyo inayotarajia kuanza Agosti 26 ikishirikisha jumla ya timu 16

Dar es Salaam. Kocha wa Azam FC, Aristico Cioaba amesema timu yake iko tayari kwa michezo ya Ligi Kuu Bara.

Azam iliweka kambi ya siku 10 nchini Uganda kujiandaa na ligi hiyo inayotarajia kuanza Agosti 26 ikishirikisha jumla ya timu 16.

Akizungumza na MCL Digital baada ya kurejea nchini Cioaba alisema ziara ya timu yake ilikuwa ya mafanikio na kusisitiza vijana wake wameiva kukabiliana na kila timu watakayokutana nayo.

“Tulicheza mechi tano na kushinda tatu na kutoka sare mechi mbili, tumerudi Tanzania kufanya maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya kwenda Mtwara lakini kiujumla nimefurahishwa na timu katika meneo yaote,”alisema Cioaba, aliyechukua jukumu la kuinoa timu hiyo mwezi Januari.

Katika hatua nyingine, raia huyo wa Romania alisema anajivunia wachezaji watano waliopandishwa kutoka timu ya vijana na anaamini watakuwa na mchango mkubwa kwa timu yake.

“Hata tuliowasajili  Mbaraka, Wazir na Salmin ni vijana ambao msimu uliopita walifanya vizuri. Kwahiyo ukiongeza na akina Yahya, Kapombe, Elias ninaamini watasaidia sana,”alisema

Wachezaji waliopandishwa ni Yahya Zaid, Abbas Kapombe, Godfrey Elias, Mohammed Omary na Stanslaus Ladislaus ambao wana kibarua cha kurejesha hadhi ya Azam msimu ujao.

Kibarua cha kwanza cha chipukizi hao kitakuwa kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda, katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Agosti 26.

Wakati huohuo, kipa wa Azam, Metacha Mnata amerejea kwenye kikosi hicho baada ya kushindwa kukamilisha usajili wa kujiunga na Mbao FC kwa mkopo.

“Mpaka dirisha dogo ndio nitajiunga na Mbao, kwa sasa nimerudi Dar kuungana na wenzangu kujiandaa na Ligi kuu,” alisema Mnata aliyepandishwa kwenye kikosi cha kwanza msimu uliopita.