Ghana yazima malumbano ya posho

Muktasari:

Shirikisho la Soka Ghana lilisema wachezaji walitaka kuonyesha kuwa wapo tayari kwa ajili ya kupigania taifa lao na si fedha pekee zinazoweza kuwahamasisha.

Franceville, Gabon. Kikosi cha Ghana kimekubali kupokea kiasi chochote cha fedha kitakachotolewa na serikali yao kama bonasi ili kuepusha migogoro kama iliyopita.

Shirikisho la Soka Ghana lilisema wachezaji walitaka kuonyesha kuwa wapo tayari kwa ajili ya kupigania taifa lao na si fedha pekee zinazoweza kuwahamasisha.

Katika fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, Serikali ya Ghana ilitoa zaidi ya Dola 3 milioni (Pauni 1.8 milioni) zikiwa taslimu zilizosafirishwa kwa ndege kwenda kwa wachezaji. Pia, kulikuwa ma mgogoro wa bonasi 2010.

Ghana ilitinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini, lakini mafanikio hayo yalizimwa na matatizo ya bonasi ya Dola 63,000 zilizoahidiwa kwa kila mchezaji. Baadhi ya mashabiki wa Ghana walionyesha hasira yao juu ya matatizo hayo ya bonasi, huku wengine wakiwataka wachezaji kujali utaifa kwanza.

Kikosi cha sasa kimeahidi kuangalia kwanza masilahi ya timu na kuwapa furaha mashabiki wao na kucheza soka la kuvutia nchini Gabon.

Ghana wapo katika kampeni ya kutwaa taji la tano la Afrika baada ya kuifunga Uganda bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi D, Jumanne.