Isihaka apewa mikoba Mbonde

Muktasari:

  • Mtibwa Sugar imeondokewa na wachezaji wake watatu wa kikosi cha kwanza waliohamia Simba ni Mbonde, kipa Said Mohammed na  beki Ally Shomari.

Dar es Salaam. Kocha wa  Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema beki Hassan Isihaka ndiye mrithi sahihi wa Salim Mbonde aliyetimkia Simba.

Mtibwa Sugar imeondokewa na wachezaji wake watatu wa kikosi cha kwanza waliohamia Simba ni Mbonde, kipa Said Mohammed na  beki Ally Shomari.

Tayari Mtibwa imemrejesha Shaban Kado kuziba pengo la  Moahmmed wakati Salum Kanoni akichukua nafasi ya Shomari na sasa imemsajili  Isihaka kuziba nafasi ya Mbonde.

Katwila alisema kutokana na uwezo wa Isihaka anaamini ataitendea haki nafasi hiyo msimu ujao na kuhakikisha Mtibwa Sugar inakuwa imara kwenye safu ya ulinzi.

"Isihaka ni mmoja wa mabeki wazuri nchini na ndio maana nimemjumuisha katika kikosi changu ili kuziba pengo la Mbonde aliyehamia Simba. Najua ataitendea haki nafasi hiyo na kuhakikisha safu ya ulinzi inakuwa imara muda wote msimu ujao.

Alisema bado anaendelea kukiimarisha kikosi chake wakati huu dirisha la usajili linaelekea kufungwa na naamini atakuwa na kikosi bora licha ya wachezaji wake wengi kuihama timu hiyo.

"Bado tuko imara tutakuja kivingine msimu ujao, watu watarajie kuona  soka la kisasa kutoka ndani ya timu hii kwani usajili wetu tuliofanya umezingatia mapungufu ya msimu uliopita"alisema Katwila.

Isihaka aliichezea African Lyon msimu uliopita pia alihusishwa  kutakiwa na Kagera Sugar na Ndanda kabla ya kujiunga na miamba hiyo ya Turiani Morogoro.