JKT Oljoro yalia kupewa kundi la kifo FDL

Muktasari:

  • Massawe alisema moja ya timu zitakazompa ushindani mkubwa katika Kundi C ni  Toto African yenye historia ya kushuka na kupanda msimu unaofuata kutokana na kubaki na kikosi chake kile kilichoshiriki Ligi Kuu.

Arusha: Kocha Mkuu wa  JKT Oljoro,  Emmanuel Massawe amesema wamepangwa kundi la kifo  katika ligi daraja la kwanza (FDL) msimu ujao.

Massawe alisema moja ya timu zitakazompa ushindani mkubwa katika Kundi C ni  Toto African yenye historia ya kushuka na kupanda msimu unaofuata kutokana na kubaki na kikosi chake kile kilichoshiriki Ligi Kuu.

“Toto African ni timu nzuri imeundwa na wachezaji wenye uzoefu wa kucheza ligi mbalimbali hasa ligi daraja la kwanza na ligi kuu, hii ndio sababu tunaiona kuwa ndio timu pekee itakayotuletea ushindani,” alisema Massawe.

Aliongeza kundi lingine litakalokuwa na ushindani ni Kundi A lenye timu za African Lyon (Dar), Ashanti United (Dar), Friends Rangers (Dar), JKT Ruvu (Pwani), Kiluvya  United (Pwani), Mgambo JKT (Tanga), Mvuvunwa na Polisi Moro (Moro).

Timu zinazounda Kundi C, Alliance School  (Mwanza), Rhino Rangers (Tabora), Pamba (Mwanza), Polisi Mara (Mara), Polisi Dodoma  (Dodoma), Transit Camp (Shinyanga), Toto  African (Mwanza), JKT Oljoro (Arusha).