JPM kujenga uwanja kisasa Dodoma

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akiwa na ndoto za kuhamishia Serikali yake mjini Dodoma, kiongozi huyo mkuu wa nchi ameamua kuacha kumbukumbu kupitia uwanja wa kisasa wa michezo.

Jana, Rais Magufuli alieleza kuwa amemuomba mgeni wake, Mfalme Mohammed VI wa Morocco kuijengea Tanzania uwanja mkubwa wa kisasa wa michezo Dodoma. Alisema  maombi hayo yamekubaliwa na kiongozi huyo wa Morocco.

Magufuli aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam katika  mazungumzo maalumu na  mgeni wake huyo aliyetua nchini  juzi kwa ziara  ya siku tatu, ikiwamo utiaji saini wa makubaliano ya biashara na Tanzania pamoja na likizo ambayo atatumia kutembelea vivutio  vya utalii.

Magufuli alimtaka mfalme huyo ambaye nchi yake imepiga hatua katika medani ya michezo, ikiwamo soka kuijengea Tanzania uwanja mkubwa zaidi ya ule wa Taifa uliopo jijini Dar es Salaam.

Mfalme Mohammed VI alijibu kuwa amekubali maombi hayo na kuahidi kujenga uwanja huo  kwa  Dola  100 milioni, sawa na  zaidi ya Sh200 bilioni za Tanzania.

Ingawa mipango halisi ya ujenzi huo wa kisasa haijaelezwa, endapo utakamilika wakati Rais Magufuli akiwa bado madarakani atakuwa amejijengea sifa na jina kama ilivyokuwa kwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyeahidi kujenga  uwanja wa  kisasa, kwa sasa ndiyo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ujenzi wake ulifanywa kwa msaada wa Serikali ya China.

Uwanja  huo uligharimu  Sh56 bilioni na  una uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 kwa wakati mmoja  ukiwa pia na ofisi, viwanja vya michezo mingine, ambavyo havijakamilika na kutumika.