Joe Hart kama mfalme nyumbani

Joe Hart

Muktasari:

Hart, ambaye anatarajia kuondoka Manchester City huku Claudio Bravo akikaribia kusaini, alikuwa na kazi wakati alipopewa beji ya unahodha dhidi ya Steaua Bucharest katika mchezo wa marudiano ya kufuzu kwa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Manchester, England. Joe Hart ameanza kwa mara ya kwanza msimu huu na unaweza kuwa mchezo wake wa mwisho kuitumikia Manchester City, akitoka bila kuruhusu bao kwa kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola.

Hart, ambaye anatarajia kuondoka Manchester City huku Claudio Bravo akikaribia kusaini, alikuwa na kazi wakati alipopewa beji ya unahodha dhidi ya Steaua Bucharest katika mchezo wa marudiano ya kufuzu kwa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ikiongoza kwa mabao 5-0 kutoka kwenye mchezo wa kwanza, Manchester City waliamua kupumzisha baadhi ya nyota wao wa kikosi cha kwanza.

Bao la kichwa la Fabian Delph lilitosha kuipa Man City ushindi wa nyumbani wa 1-0, akitumia vizuri mpira wa krosi ya Jesus Navas, na kufanya matokeo ya jumla kuwa 6-0.

Hata hivyo, kocha wa Man City alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari kuwa Hart angeanza katika mchezo huo na kupewa majukumu yake ya unahodha.

Kila alipogusa mpira, kipa huyo wa miaka 29 alikuwa akishangiliwa na mashabiki wa klabu hiyo huku kukiwa na mabango mengi yenye ujumbe wa kumsapoti kipa huyo namba moja wa England.

Dakika ya 66 ya mchezo huo wa 348 kwa Hart, wakati mchezaji wa Steaua Bucharest akiagwa, umati katika Uwanja wa Etihad ulisimama na kuimba ‘Simama kama unampenda Joe Hart’.

Kipa huyo aliwajibu mashabiki hao waliokuwa wamesimama huku wakipiga makofi na kuimba jina lake kwa kutikisa kichwa na kupigapiga nembo ya klabu aliyokuwa ameivaa.

Hart alikuwa na kazi kidogo ya kufanya wakati wenyeji wakitafuta bao la kusawazisha.

Aliokoa baadhi ya michomo ya hatari, akipangua mipira kwa miguu huku akimsahihisha Guardiola kwa kukataa shambulizi la Nicolae Stanciu kwa mkwaju wa adhabu na lile la Alexandru Tudorie.

Alishangilia kwa nguvu pia bao la Delph kwa kunyoosha mikono yake juu na kuirusha kwa nguvu.

Baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo, Hart alizunguka katika pande zote nne za Uwanja wa Etihad pamoja na wachezaji wenzake wakishangilia ushindi.