Katiba yaigomea Yanga Yetu ya Manji

Makao makuu ya klabu ya Yanga.

Muktasari:

  • Katiba ya Yanga ya 2010 inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ibara ya 56, ibara ya 56, ibara ya 56 inatambua suala la klabu hiyo kubadilika kuwa kampuni ya umma na siyo mali ya mtu mmoja au kikundi.

Dar es Salaam. Mchakato unaofanywa na klabu ya Yanga wa kutaka kukodisha nembo na timu hiyo kwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji unakwenda kinyume na Katiba ya klabu hiyo kongwe nchini.

Katiba ya Yanga ya 2010 inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ibara ya 56, ibara ya 56, ibara ya 56 inatambua suala la klabu hiyo kubadilika kuwa kampuni ya umma na siyo mali ya mtu mmoja au kikundi.

Ibara ya 56 yenye kichwa cha habari, Kampuni ya Umma ya Yanga inaonyesha jinsi klabu hiyo itakavyofuata utaratibu wa kubadilika na kuingia katika mfumo wa kampuni.

Ibara ya 56 (1), inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young Africans Corporation Limited itakayosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni ikiwa kampuni ya umma yenye hisa.

Ibara ya 56(2), “Wanachama wote ambao katika tarehe ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2007 wako hai, watakuwa, kwa nguvu ya uanachama wao, wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakazopata kwa mujibu wa mwafaka wa Yanga uliofikiwa Juni 6, 2006.

Ibara ya 56 (3) inasema, “Klabu itamiliki hisa zilizo sawa na asilimia hamsini na moja (51) ya hisa zote zilizopo katika kampuni.

Ibara ya 56 (4) inasema,” Mkutano mkuu wa uchaguzi utachagua wanachama wawili ambao siyo miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurungenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha masilahi ya klabu kwenye kampuni.

Hivyo, uamuzi wa Manji kuanzisha kampuni, Yanga Yetu Limited anayoimiliki kwa asilimia 99 na kukodisha timu na nembo ya klabu hiyo kwa kipindi cha miaka kumi unapingana na Ibara 56 (3) inayotoa nafasi kwa klabu kumiliki asilimia 51 za hisa.

Maoni ya wadau

Ofisa habari na mawasiliano wa TFF, Alfred Lucas alisema shirikisho hilo linaunga mkono mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu, lakini lazima yazingatie katiba ya klabu husika pamoja na kanuni na taratibu za uendeshaji soka.

“TFF haipingi mabadiliko yanayotaka kufanywa na Yanga tunapongeza, lakini tunasisitiza lazima wafuate utaratibu,” alisema Lucas.

Mwanachama Hassan Msigiti aliyekutwa maeneo ya Jangwani alisema hakuna wa kukwamisha mchakato wa kumpa timu Manji kwani wanachama walishaamua.

“Wanaopiga kelele waje mkutanoni...hao TFF mikataba yao haipo wazi, leo waje kuiingilia Yanga. Safari hii tumeshaamua na hakuna wa kutuzuia. Wewe (mwandishi) subiri uone,” alisema Msigiti na kuungwa mkono na Daud Almas, mwanachama mwenye kadi namba 474.

Aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji, Salum Mkemi alisema mkutano huo wa dharura ni batili, akipinga pia mpango wa timu hiyo kukodishwa bila kufuata taratibu na kusema yeye na wenzake waliovuliwa nyadhifa zao na kufukuzwa uanachama bado ni wanachama halali wa klabu hiyo.

Mgogoro kama huo uliwahi kutokea 1986 ukasababishia Yanga ishindwe kuutetea ubingwa wake na ulipamba moto zaidi 1987, huku pande mbili zikipingana, uongozi uliojiita Yanga-Ukuta na wanachama waliojiita Yanga-Katiba.