Keane ampa ushauri wa bure Wenger

Muktasari:

Keane alisema hayo baada ya kushuhudia Ozil juzi usiku akifunga mabao matatu ‘hat-trick’ kwa mara ya kwanza akiichezea klabu hiyo ya Emirates kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Sanchez akifunga bao tamu la kuongoza kwa vijana hao wa Wenger walipoiangamiza Ludogorets 6-0.

London, England. Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane ameshauri kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kuharakisha mikataba mipya kwa nyota wake, Mesut Ozil na Alexis Sanchez ili kuepuka janga la kuwapoteza.

Keane alisema hayo baada ya kushuhudia Ozil juzi usiku akifunga mabao matatu ‘hat-trick’ kwa mara ya kwanza akiichezea klabu hiyo ya Emirates kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Sanchez akifunga bao tamu la kuongoza kwa vijana hao wa Wenger walipoiangamiza Ludogorets 6-0.

Wawili hao walisaidiana katika mabao yao na wameendelea kuwa na msimu mzuri kiasi cha kuiwezesha Arsenal kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) ikiwa na pointi sawa na Manchester City na kuongoza Kundi A la Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa kwa idadi ya mabao.

Kwa pamoja, Ozil na Sanchez mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu wa 2018, kulingana na maelezo ya Wenger, wameiambia klabu hiyo kuwa watazungumzia hatima zao klabuni hapo kutegemea na matokeo ya klabu hiyo kwenye mashindano mbalimbali, wala nia zao siyo kushawishiwa kwa fedha.

Keane alisema: “Ninafikiri aina ya wachezaji hao ni nadra kuwa nao, wanaweza kuifikisha klabu yao kwenye mafanikio mkubwa wakiongeza juhudi, suala la fedha kwao siyo jambo la msingi kwani wao siyo masikini tena wanaweza hata kuacha soka na wakaendelea kuishi vizuri. “Kama klabu (Arsenal) lazima ijitahidi kuendelea kuwa nao kwa mafanikio zaidi kinyume chake wanaweza kwenda kwa maadui zao.”

Taarifa mbalimbali zimekuwa zikieleza Ozil na Sanchez wamedai mishahara inayofikia Pauni 250,000 kwa wiki ili kusaini mikataba mipya na klabu hiyo wanayotaka kuitumikia hadi 2020.

Keane, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa masuala ya soka wa kituo cha televisheni cha ITV, alieleza umuhimu wa Arsenal kuwabakiza nyota hao.

“Kujaribu kupata saini ya Ozil ni jambo la msingi kwa klabu kama ilivyo kwa mwenzake, Sanchez, kwani mchango wao unaonekana dhahiri Ligi Kuu na ile ya Mabingwa Ulaya.

Mechi zijazo za Arsenal:

Ligi ya Mabingwa-

Ludogorets (Ugenini) - Novemba 01.

PSG (Nyumbani) - Novemba 23.

FC Basel (Ugenini) – Desemba 6.