Kichuya, Mavugo waizima Yanga

Muktasari:

Ushindi huo unaifanya Simba kuongoza kwa Ligi Kuu kwa pointi 54 na kuiacha Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 49.

Vinara wa Ligi Kuu, Simba wakicheza pungufu wamefanikiwa kuichapa Yanga kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo mabao ya Simba yalifungwa na Laudit Mavugo na Shiza Kichuya wakati bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Simon Msuva kwa mkwaju wa penalti.

Ushindi huo unaifanya Simba kuongoza kwa Ligi Kuu kwa pointi 54 na kuiacha Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 49.

Katika mchezo huo Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao kwa penalti baada ya beki wa Simba, Novalty Lufunga kumwangusha kwenye eneo la hatari mshambuliaji Obrey Chirwa bao lililodumu hadi mapumziko.

Simba ilianza vibaya kipindi cha pili kwa beki wake Abdi Banda kupewa kadi nyekundu katika dakika 55, na mwamuzi Mathew Akrama kwa kumshika Amissi Tambwe wa Yangaaliyekuwa akielekea golini kufunga.

Kocha wa Simba alilazimika kuwapumzisha Lufunga, Luizio na Mohamed Ibrahim na kuwaingiza Kichuya, Said Ndemla na Jonas Mkude.

Mabadiliko yaliyoisaidia Simba kupata mabao yake mawili

Mavugo anaisawazishia katika dakika 65, akiunganisha krosi ya Kichuya kabla ya Kichuya kupachika bao la pili la ushindi katika dakika 80 na kupeleka majonzi Jangwani.