Kikosi dhaifu kiliiathiri Yanga Kombe la CAF

Muktasari:

Ilikuwa na wachezaji 25 kwa ajili ya mashindano hayo makubwa

Dar es Salaam. Wakati Yanga ikihitimisha mechi zake sita za hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe wiki iliyopita, wachezaji wanne kwenye kikosi chake walishindwa kucheza hata mechi moja.

Wachezaji hao ni makipa Benno Kakolanya na Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Pato Ngonyani na mshambuliaji Malimi Busungu.

Takwimu za utendaji Yanga zinaonyesha kuwa wachezaji hao walishindwa kucheza walau dakika moja kwenye hatua hiyo ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) ambalo Yanga ilipangwa Kundi A pamoja na TP Mazembe, MO Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Kipa Deogratias Munishi ‘Dida’, beki Mbuyu Twite na kiungo Thabani Kamusoko ndio walikuwa vinara wa mechi nyingi kwenye kikosi hicho baada ya kucheza mechi zote sita, sawa na dakika 540.

Mshambuliaji Amissi Tambwe aliwafuatia kwa kucheza dakika nyingi, 466, akisogelewa na Obrey Chirwa, dakika 431.

Mkongwe Kelvin Yondani alicheza dakika 390, Vincent Bossou na Donald Ngoma, kila mmoja akicheza dakika 360.

Mbali ya Busungu, Kakolanya, Barthez na Ngonyani, wengine waliocheza kwa muda mfupi katika hatua hiyo na dakika zao kwenye mabano ni; Matteo Anthony (23) na Geofrey Mwashiuya (41).

Wengine ni; Andrew Vincent ‘Dante’ (90), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (90), Hassan Kessy (90) na Said Juma ‘Makapu’ (123).

Kutokana na kuwapo kundi la wachezaji ambao hawakucheza kwa muda mrefu katika hatua hiyo, Yanga ililazimika kuwatumia baadhi ya wachezaji mara kwa mara kutokana na ufinyu wa kikosi chake chenhye wachezaji 25. Kocha Hans Pluijm alikiri kuwa ufinyu wa kikosi chake ni miongoni mwa mambo yaliyoigharimu timu hiyo kwenye hatua hiyo ya makundi.

“Nina kikosi kidogo na ndiyo maana unaona nimekuwa nikifanya mzunguko katika kuwatumia wachezaji walewale ili angalau wengine wapate nafasi ya kupumzika,” alisema.