Kim awasoma wabaya Serengeti

Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Soka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kim Poulsen

Muktasari:

  • Serengeti Boys imepangwa Kundi B  pamoja na Angola, Niger na mabingwa watetezi Mali katika fainali za Mataifa ya Afrika zitakazoanza Mei 26 hadi Juni 4 mwaka huu nchini Gabon.
  • Akizungumza na gazeti hili, Kim alisema atatumia njia mbalimbali kupata taarifa za wapinzani wao kabla ya kwenda Gabon.

Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Soka katika  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kim Poulsen amesema ameanza kusaka taarifa kuhusu timu za taifa za vijana za Niger, Angola na Mali.
Serengeti Boys imepangwa Kundi B  pamoja na Angola, Niger na mabingwa watetezi Mali katika fainali za Mataifa ya Afrika zitakazoanza Mei 26 hadi Juni 4 mwaka huu nchini Gabon.
Akizungumza na gazeti hili, Kim alisema atatumia njia mbalimbali kupata taarifa za wapinzani wao kabla ya kwenda Gabon.
“Tunatumia mbinu tofauti kupata taarifa na hatujalala.
Mali ni mabingwa watetezi, Angola na Niger pia ni wazuri, sasa kuna ulazima wa kupata taarifa zao, tutatumia kila njia kupata kanda za video za michezo yao,” alisema Poulsen.
Katika hatua nyingine kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars aliweka wazi kuwa benchi la ufundi lina mitazamo miwili kuhusu michezo ya kirafiki.
“Kwanza tunaangalia kama tutapata mwaliko wa mashindano ya kimataifa kama ilivyokuwa India au kucheza mechi za kimataifa za kirafiki,” alisema Poulsen.
Ikiwa katika harakati za mechi za mchujo Serengeti ilialikwa
India ambako ilicheza mechi za kujipima nguvu na nchi za Marekani, Korea Kusini, India na Malaysia.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime aliripoti kambini jana kuanza kukinoa kikosi hicho.
Shime alikuwa akiinoa Ruvu JKT ambayo inayofanya ovyo Ligi Kuu.