Kipa Burhan kuzikwa Iringa

Marehemu David Burhani alipokuwa na kikosi cha Mbeya City kabla ya kwenda Majimaji na baadaye Kagera Sugar. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Burhan alifariki dunia jana asubuhi katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza alipokuwa amelazwa kwa takribani siku tatu akisumbuliwa na malaria.

Mwanza. Uongozi wa Kagera Sugar umesema mwili wa kipa wao, David Burhan aliyefariki dunia jana utasafirishwa leo kwenda kwao Iringa kwa mipango ya mazishi.
Burhan alifariki dunia jana asubuhi katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza alipokuwa amelazwa kwa takribani siku tatu akisumbuliwa na malaria.
Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein alisema mwili wa marehemu utasafirishwa leo kuelekea mkoani Iringa na shughuli za mazishi zitapangwa na familia yake. “Hatutausafirisha mwili leo (jana) kutokana na kuwa na mechi ya Ligi Kuu, hivyo utaratibu utakuwa kesho (leo) na suala la mazishi litapangwa na familia yake,” alisema Meneja huyo.
Hussen aliongeza kusema kifo cha Burhan pigo na kusikitisha kwani anakumbuka katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida United walikuwa naye safarini.
“Alikuwa akisumbuliwa na malaria takribani siku tatu, hii imekuwa pigo kubwa kwa timu na taifa kwa ujumla haswa kwenye tasnia ya michezo, lakini yote ni mipango ya Mungu,” alisema Hussein.
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema ni huzuni usiyoisha leo na kuongeza kuwa hana mengi tofauti na kuumizwa na tukio hilo.
“Niseme tu kwamba ni pigo, ni pigo na ni pigo..sina mengi zaidi,” alisema Mexime kwa kifupi.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA), Salum Chama alisema wamepokea msiba huo kwa masikitiko, hivyo wataungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.
“Kwa ujumla sisi kama uongozi wa mkoa, tumesikitika sana, lakini niseme kwamba tutashirikiana na familia ya marehemu na uongozi mzima wa timu kuhakikisha tunamfikisha sehemu yake ya mwisho,” alisema Chama.
 Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kutuma salamu zake za pole kwa familia ya marehemu na klabu ya Kagera Sugar.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha David Abdalah Burhan mchezaji wa Kagera Sugar. Amefariki usiku wa kuamkia leo. Apumzike kwa amani,” aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.
Burhan ni miongoni mwa wachezaji walioisadia Mbeya City kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakati wa msimu wake wa kwanza kushiriki ligi hiyo kabla ya kutimkia Majimaji na baadaye Kagera Sugar.