Kipa atoa siri uchawi wa Ngaya

Muktasari:

Mmadi alisema hakuna uchawi wowote alioweka golini, lakini alitaka kuwavuruga akili wachezaji wa Yanga ili wahamaki na washindwe kuwafunga mabao mengi.


Dar es Salaam. Kipa wa Ngaya Club ya Comoro, Said Mmadi amesema alitaka kuwateka akili wachezaji wa Yanga kwa kuamini alifukia kitu golini na anashukuru alifanikiwa.

Mmadi alisema hakuna uchawi wowote alioweka golini, lakini alitaka kuwavuruga akili wachezaji wa Yanga ili wahamaki na washindwe kuwafunga mabao mengi.

Mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Ngaya uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 ulitawaliwa na dhana ya imani za kishirikina mwanzo hadi mwisho wa mchezo.

Wakati Yanga wakilishambulia goli la Ngaya na kukosa mabao waliamini kuwa langoni kwa wapinzani wao kuna kitu kimefukiwa na ndiyo maana hawapati mabao.

Dakika ya 30 baada ya Yanga kukosa bao, Obrey Chirwa alionekana akifukua kitu na kukitupa nje uwanja.

Pia, dakika ya 42 beki wa Yanga, Vincent Bossou alionekana akiinama golini kwa Ngaya karibu na mlingoti wa goli akifukua kitu ambacho hata hivyo hakukiona.

Baada ya mapumziko wakati timu zikirudi uwanjani, kipa wa Ngaya, Mmadi alionekana akichuchumaa na akichimba udongo na kama anafukia kitu golini kwake.

Wakati kipa huyo akifanya hivyo, wachezaji wote walikuwa wakimtazama kwa makini huku mwamuzi Alex Muhabi kutoka Uganda akimtazama pia na alipomaliza kufanya mambo yake na kusimama mwamuzi akapuliza filimbi kuashiria kipindi cha pili kuanza.

Hali hiyo ilionekana kama kuzidi kuwachanganya wachezaji wa Yanga ambao jana walikosa mabao mengi na dakika ya 56, Deus Kaseke alionekana akifukua kitu golini na kufanya ishara kama ana kitupa nje ya uwanja.

Mmadi aliliambia gazeti hili kuwa hata hakuweka kitu golini na alichofanya ni kuwavuruga kisaikolojia wachezaji wa Yanga ikiwa ni mbinu yake ya mchezo na anashukuru alifanikiwa na mechi kuisha kwa sare.

“Unajua sisi ni mara ya kwanza kushiriki mashindano kama haya. Kule kwetu Yanga walitufunga mabao 5-1 na walitamba kuwa huku kwao watatupiga saba.

“Nikaona ili wasitufunge mabao mengi nifanye kitu kuwavuruga na kweli niliwashinda kwani walihamaki na kuonekana kama wanahisi kuna kitu nilifukia golini ndiyo maana wanakosa mabao, kumbe hakuna chochote ni mbinu ya mchezo tu,” alisema Mmadi.

Aliongeza: “Nafurahi kwa sare hii kwani ni kama ushindi kwetu. Tunafurahi kwani kila mara tumekuwa tukiimarika na natumaini mashindano yajayo hatutakuwa kama sasa.”