Kuwait kujenga uwanja wa michezo Mburahati

Muktasari:

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasen Al Najem wakati wa kukabidhi visima viwili vyenye thamani ya Sh 12 milioni vya maji salama kwa shule hizo mbili kupitia mradi wa kisima cha maji kwa kila shule hapa.

Dar es Salaam. Ubalozi wa Kuwait umeahidi kujenga uwanja wa soka na wavu katika shule ya msingi Barafu na Sekondari ya Mburahati ili kuendeleza michezo nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasen Al Najem wakati wa kukabidhi visima viwili vyenye thamani ya Sh 12 milioni vya maji salama kwa shule hizo mbili kupitia mradi wa kisima cha maji kwa kila shule hapa.

Najem alisema kuwa wanatambua umuhimu wa michezo kwa wanafunzi na wamedhamilia kuanza mradi huo mara baada ya kukamilisha taratibu mbalimbali.

Amesema kuwa serikali ya Kuwait inaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ya kuondoa changamoto mbalimbali.

“Hii ni moja ya shughuli zetu za kudumisha ushirikiano baina ya serikali ya Kuwait na Tanzania, tunajua umuhimu wa michezo na sekta nyingine na kuamua kuongeza nguvu kuondoa changamoto hizo, naipongeza taasisi ya Tanzania Holy Quran Memorization Charitable Trust chini ya Sheikh Othman Ally Kaporo kwa kuratibu shughuli hii,” alisema Najem.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Barafu, Isidory Kibassa ameushukuru uongozi wa ubalozi wa Kuwait na taasisi ya Tanzania Holy Quran Memorization Charitable Trust kwa ahadi ya ujenzi wa uwanja na kukabidhi visima vya maji.

Kibassa alisema kuwa elimu ya darasani na michezo ni vitu vinavyoendana na kuomba wadau kuunga mkono juhudi za Ubalozi wa Kuwait kwani bado shule yao ina changamoto mbalimbali.