Leicester , Real zakata tiketi ya 16 bora Ulaya, Spurs nje

Muktasari:

Hata hivyo, Tottenham au Spurs kutoka England ilitupwa nje ya hatua hiyo kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.

London, England. Klabu ya Leicester City imeendeleza rekodi yake safi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji juzi na kufuzu kucheza hatua ya mtoano, ikiungana na mabingwa wa kihistoria, Real Madrid.

Hata hivyo, Tottenham au Spurs kutoka England ilitupwa nje ya hatua hiyo kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.

Leicester, washiriki kwa mara ya kwanza waliungana nao; Juventus, Bayer Leverkusen na Monaco kufuzu.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England waliungana na washindi wa pili kwa mwaka jana, Atletico Madrid, Arsenal, Paris Saint-Germain, Bayern Munich na Borussia Dortmund, ambazo zilikuwa tayari zimefuzu, ambako mechi za jana usiku zilitarajiwa kutoa wawakilishi wawili zaidi, ambao huenda ni Barcelona, Manchester City.

Leicester ilifuzu kutoka G kama mshindi wa kwanza, jambo lililoiwezesha izikwepe klabu kubwa Ulaya kwenye hatua inayofuata, ambako kocha Claudio Ranieri alikenua meno kwa furaha. Vijana hao wa Ranieri wapo pointi mbili kutoka mstari wa kushuka daraja kwenye Ligi Kuu England (EPL).

“Tupo kwenye safari nyingine. Sijui ni wapi tuendako, lakini tumefurahi!” alieleza Ranieri baada ya mchezo huo.

Kuhusu kiwango duni kwenye EPL msimu huu, kocha huyo, raia wa Italia alieleza: “Pengine ni kwa sababu tuliwekeza akili, nguvu zetu nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa sasa, tumemaliza kazi, tumeongoza kundi letu, ni muhimu kurudisha akili zetu kwenye ligi.”

Mshambuliaji wake, raia wa Japan, Shinji Okazaki alifunga bao la mapema, dakika ya tano na kufuatiwa na la pili la winga wa Algeria, Riyad Mahrez kwa penalti, lakini Jose Izquierdo alifunga la kufutia machozi kwa Brugge.

“Tulitaka kuongoza kundi letu. Haikuwa kazi rahisi, lakini tumeweza,” alisema nyota huyo wa Algeria.

Bao la mshambuliaji, raia wa Colombia, Izquierdo, lilikuwa la kwanza ambalo Leicester imeruhusu kwenye mashindano hayo msimu huu.

Wakati Leicester ikishangilia, Tottenham iligonga mwamba baada ya kufungwa mabao 2-1 na AS Monaco ya Ufaransa, iliyotwaa uongozi Kundi E.

Spurs ilianza vyema kwa kipa wao Mfaransa Hugo Lloris kuzuia mkwaju wa penalti wa Radamel Falcao. Lakini, mabao ya haraka ya Djibril Sidibe na Thomas Lemar baada ya kuanza kwa kipindi cha pili yalifuta lile la Spurs kwa mkwaju wa penalti wa Harry Kane.

Kwenye mchezo wa kundi hilo, Bayer Leverkusen ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya CSKA Moscow na kukata tiketi iliyobaki ya kucheza mtoano ikisaidiwa na kupoteza kwa Spurs.

Kevin Volland aliipa bao la kuongoza Leverkusen, dakika ya 16 kabla ya Mwisraeli, Bibras Natcho kusawazisha.

Spurs itakamilisha hatua ya makundi kwa kuikaribisha CSKA, Desemba ambako matokeo hayo yataamua timu ipi iende Ligi ya Europa . Mchezo huo kwenye Uwanja wa Wembley utakuwa mtihani kwa kocha Mauricio Pochettino, ambao wameharibiwa na kufunga na Monaco na Leverkusen kwenye uwanja huo.

“Nimeumizwa. Tulitaka kwenda mbele zaidi, lakini ni bahati mbaya tumekwama. Tutakamilisha mchezo wetu kwa kufanya vizuri, tunatumaini kucheza Ligi ya Europa.” Kane aliiambia BT Sport.

Mabingwa mara 11, Real Madrid walijiunga na washindi wa mwaka 1997, Borussia Dortmund kufuzu kutoka Kundi F baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sporting Lisbon, aliyokulia nyota wao, Cristiano Ronaldo.

Beki Raphael Varane alifungua milango kwa wageni, Real, lakini Mbrazili, Adrien Silva alifunga kwa penalti, huku mtokea benchi Karim Benzema akimaliza kazi kwa Real, usiku ambao Ronaldo alishindwa kuweka rekodi mpya ya mabao 100.

Siku 11 kabla ya kuikabili Barcelona kwenye mchezo wa El Clasico, Desemba 3, Real ilipata pigo baada ya winga wake, Gareth Bale kuumia.

“Tulijua utakuwa mchezo mgumu kwetu, lakini tumefarajiwa na pointi tatu muhimu,” alisema kocha wa Real , Zinedine Zidane, ambaye mwaka 2002 alikuwa mchezaji wa klabu hiyo. Zidane alianza kuinoa Real tangu Mei.

Rekodi ya mabao

Dortmund iliyokuwa tayari imefuzu, ilitwaa uongozi wa kundi hilo kwa karamu ya mabao licha ya kubakiza mchezo wa mwisho baada ya kuitandika Legia Warsaw ya Poland 8-4 , rekodi ya mabao mengi kwenye ligi hiyo.

Hadi mapumziko, matokeo yalikuwa mabao 5-2. Marco Reus alifunga matatu ‘hat-trick’, nyota wa Japan, Shinji Kagawa mawili.

Nao mabingwa mara mbili, Juventus walifuzu baada ya kuwafunga mabao 3-1 vinara wa Kundi H Sevilla, ambao ni mabingwa wa Ligi ya Europa kwa misimu mitatu katika ardhi yao, Hispania.

Claudio Marchisio alifunga kwa penalti, Leonardo Bonucci na Mario Mandzucic waliifungia klabu hiyo, Kibibi Kizee cha Turin ambako Nicolas Pareja aliifutia Sevilla machozi.

Jana, Barcelona na Manchester City zilikuwa zikicheza kwa matumaini ya kukamilisha timu 16 zilizofuzu kwa hatua ya mtoano zikicheza dhidi ya Celtic na Borussia Moenchengladbach.