Liewig atoboa siri ya kuituliza Yanga

Kocha wa Stand United, Patrick Liewig.

Muktasari:

  • Mfaransa huyo anayeamini katika soka la wachezaji chipukizi alisema hayo baada ya kikosi chake kuichapa Yanga bao 1-0 Jumapili kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Shinyanga. Kocha wa Stand United, Patrick Liewig amesema licha ya timu yake kutokuwa na wachezaji wenye majina makubwa kama Yanga, bado wameonyesha watapata mafanikio msimu huu.

Mfaransa huyo anayeamini katika soka la wachezaji chipukizi alisema hayo baada ya kikosi chake kuichapa Yanga bao 1-0 Jumapili kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

“Kikosi cha Stand kimejaa vijana ambao wanahitaji mafanikio, naamini watapambana ili kufika mbali na hilo litafanikisha malengo ya klabu,” alisema Liewig.

Alisisitiza kuwa anachozingatia katika timu yake ni kuhakikisha mchezaji anakuwa na nidhamu na muda wa kuisaidia timu kufikia malengo yake.

“Bila nidhamu tusingekuwa nafasi ya pili, ambayo tumefikisha baada ya kuwafunga Yanga na hii wachezaji wangu wasije wakaona wamemaliza kazi, bado na safari ni ndefu,” alisema Mfaransa huyo.

Wakati kocha huyo akijivunia mafanikio hayo, uongozi wa klabu hiyo umeanza kutafuta kocha wa kurithi mikoba yake.

Katibu wa Stand United, Kennedy Nyangi alisema wameanza kufanya mazungumzo na kocha wao wa zamani, Matius Lule kuchukua mikoba ya Liewig.

“Kocha Liewig tunahitaji huduma yake, lakini kwa kuwa alipewa mkataba na Acacia na alikuwa analipwa Dola 4,000, za Marekani kwetu itakuwa ngumu kumpa kiasi hicho,” alisema Nyangi.

Mwenyekiti wa usajili wa timu hiyo, Joffrey Tibakienda alisema timu tishio kwa msimu huu ni Mbao, JKT Ruvu na Kagera Sugar kutokana na viwango vya hali ya juu wanavyoonyesha uwanjani.

“Licha ya Masau Bwile (Ofisa Habari wa Ruvu) kutamka kwamba maiti imefufukia kwao akiwa na maana kwamba Mbao wamezindukia kwao, si timu ya kubeza, ipo makini, tatizo ni udhamini,” alisema Tibakienda.