Lipuli SC ilivyopanda milima kwa miaka 16

Muktasari:

Lipuli ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki ligi hiyo ikipangwa Kundi A pamoja na Friends Rangers, Mshikamano na Polisi zote za jijini Dar es Salaam, Kiluvya FC (Pwani), Pamba FC ya Mwanza na African Sports ya Tanga.


Iringa. Ligi Daraja la Kwanza imefikia patamu. Lipuli ya Iringa imekuwa ya kwanza kucheza Ligi Kuu ikifuatiwa na Singida United.

Lipuli ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki ligi hiyo ikipangwa Kundi A pamoja na Friends Rangers, Mshikamano na Polisi zote za jijini Dar es Salaam, Kiluvya FC (Pwani), Pamba FC ya Mwanza na African Sports ya Tanga.

Baada ya kukamilika kwa ligi hiyo, Lipuli imepanda Ligi Kuu baada ya kuongoza kundi lake la A huku African Sports ikishuka daraja baada ya kushika mkia katika kundi hilo.

Lipuli imepanda baada ya kusota kwa misimu mitatu Daraja la Kwanza tangu iliponunua nafasi ya iliyokuwa Polisi Iringa iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza mwaka 2013.

Kupanda kwa timu hiyo kumerejesha heshima ya mkoa wa Iringa katika soka ,heshima iliyotoweka tangu mwaka 2001 takribani miaka 16 tangu ‘Wanapaluhengo’ kushuka daraja.

Katika kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri msimu huu, uongozi wa timu hiyo Mwenyekiti Abuu Changawa na katibu wake, Willy Chikweo waliunda kamati za kusaidia timu hiyo ishinde na miongoni mwa kamati hizo ni ile ya mipango na fedha iliyoongozwa na Juli Sawani.

“Kamati yangu ilikuwa na majukumu makuu matatu, kwanza ilikuwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuendesha timu, pili kufanya usajili na kutafuta kambi ya kudumu na jukumu.

“Tulianza makujumu haya Oktoba mwaka jana tukishirikiana na mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Iringa, IRFA, Cyprian Kuyava, Jesca Msambatavangu, Malkia wa timu yetu na wadau mbalimbali akiwamo Mkurugenzi wa Makampuni ya ASAS Salim Abri ambaye alitoa mchango mkubwa wa fedha za usajili,” anasema.

 

Fitina za soka zimeipandisha Lipuli

Sawani anasema, timu ilijipanga kushindana na ikafanikiwa ndio sababu ilikuwa na uwezo wa kushinda ndani na nje ya mji wa Iringa.

“Katika awamu ya kwanza timu alipata sare mbili na kupoteza mchezo mmoja na mzunguko wa pili ilipata sare moja na nyumbani na kushinda michezo yote nyumbani na ugegeni,hata wale waliolalamika walifungwa pia walipokuwa kwenye viwanja vya nyumbani kwao kwani wangelalamika wakati tulipowafungia kwao waje kulalamikia viwanja vya Iringa,” alihoji sawani na kuongeza:

Sawani anasema kamati yake imemaliza kazi na sasa inatarajia kukabidhi ripoti kwa uongozi huku ikipendekeza mambo kadhaa ikiwemo kuboresha benchi la ufundi lifanane na Ligi Kuu na kuandaa bajeti isiyopungua Sh 7 milioni kwa ajili ya kuendesha timu hiyo kwa ngazi ya Ligi Kuu Tanzania bara.

 

Kocha Lipuli anena

Kilio cha timu zilizonyingi hususani za daraja la kwanza ni ukata wa fedha, hilo nalo halikukosekana ndani ya Lipuli, lakini kocha wa timu hiyo, Richard Amatre anasema yeye na benchi lake la ufundi walijiwekea mikakati ya kushinda kila mechi na kupandisha Timu Ligi Kuu bila ya kuzifikiria hizo changamoto.

“Tulijipanga kama benchi la ufundi lililokuwa chini yangu, ninawashukuru wasaidizi wangu Julie Elieza na meneja wa timu, Salehe Mrisho kwa pamoja wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kila wakati tupo na timu na tunahakikisha inashinda katika michezo yake iwe ndani ya Iringa na hata nje ya Iringa,”anasema

“Tuliwasihi wachezaji wajitume na wafanya kazi moja ya kuhakikisha wanaingia katika rekodi ya kupandisha timu Ligi kuu na wao walituahidi iwe mvua liwe jua lazima watafanya hivyo na ndicho walichokifanya,…kikubwa katika masuala ya mpira niliwaambia ni kuwa wavumilivu na kushimakana,” anasema.

Anasema pomoja na kupanda Ligi Kuu benchi lake la ufundi linatarajia kukabidhi ripoti kwa uongozi wa timu itakayokuwa na mapendekezo mbalimbali ya kitaalamu ya nini kifanyike ili kuhakikisha timu hiyo inakuwa ya ushindani kamili ndani ya Ligi Kuu.

Kiutaratibu Ligi Kuu kila timu inapaswa kuwa angalau na wachezaji 25 wa timu ya wakubwa na wachezaji 20 wa timu B na hizi ni taratibu lazima zizingatiwe, kwa hiyo timu yenye uwezo mdogo kama Lipuli haiwezi kuacha wachezaji wote kwa wakati mmoja na kusajili wapya,” anasema Amatre.

 

Malkia wa Lipuli

Malkia wa timu hiyo ambayo aliinunua kutoka Polisi Iringa, Jesca Msambavatangu anasema wamekamilisha kazi ya kwanza ya kuipandisha timu Ligi Kuu na jukumu lilipo mbele ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ni kuhakikisha wanaweka mipango bora itakayoifanya timu hiyo kuwa ya ushindani ndani ya Ligi kuu.

“Wakazi wa Iringa wanajua maumivu waliyopata kwa miaka 17 tangu timu yao iliposhuka daraja mwaka 2001, kwa kuliona hilo mwaka 2013 Polisi walitangaza kuuza timu yao na ndipo nilipojitokeza kununua na kusaidia kukamilisha taratibu zote za usajili wa jina pale TFF,” alisema Jesca na kuongeza:

“Kwa sasa timu hii imepanda Ligi kuu ninawashukuru wadau wote kwa kujitolea kwao, jukumu tulilonalo kwa sasa ni kuweka mipango itakayosaidia kuifanya timu kuwa ya ushindani na si ya kupanda na kushuka,” anasema.

Aliwataja viongozi hao kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza, Mku wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela, Mku wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Viti Maalumu, Ritta Kabati na wadau wengine aliodai walitoa mchango mkubwa kwa timu kuelekea Ligi Kuu.

 

Mkuu wa mkoa atoa kauli nzito

Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema mtu yeyote wa Iringa atakayeacha kuishangilia Lipuli ni sawa na msaliti.

Masenza alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kuwapokea na kuwapongeza wachezaji wa Lipuli FC kwa kupanda Ligi Kuu msimu huu.

“Lipuli FC ndiyo timu ya Wanairinga na mtu yeyote atakayeonekana akishangilia timu tofauti na Lipuli FC pindi itakapocheza iwe ugenini ama uwanja wake wa nyumbani huyo atachukuliwa kuwa ni msaliti,” alisema Masena.

“Lipuli FC ni timu ya wananchi wa Iringa na ningepende hilo lieleweke na si vinginevyo, mara nyingi timu za mikoani zimekuwa zikishindwa kupiga hatua kutokana na kuathiriwa na ushabiki wa timu kubwa za Yanga, Simba na Azam,…mimi nisengependa hilo litokea mjini Iringa kwa Lipuli FC ,” alisema Masenza

Katika hatua nyingi Masenza aliagiza mwenyekiti wa kamati ya michezo mkoa wa Iringa kukutana na wadau wa mpira kuandaa mikakati itakayowezesha timu hiyo kujitegemea wakati huohuo akiwataka wakuu wa Wilaya zote mkoani hapa kukaana wadau kujadili namna watakavyosaidia timu hiyo kuleta ushindi Ligi Kuu.