Lubeya awapasha Mkude, Ajib

Muktasari:

Akizungumza na gazeti hili, katibu mwenezi wa zamani wa timu hiyo, Said Lubeya alisema nyota hao wamekuta rekodi ya mastaa waliofanya vyema na Simba kuchukua mataji ya ubingwa.

Dar es Salaam. Nyota wa Simba, Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu ambao mikataba yao ipo ukingoni na hawaonyeshi nia ya kusaini wameambiwa waende kwani wao siyo wa kwanza kuichezea timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, katibu mwenezi wa zamani wa timu hiyo, Said Lubeya alisema nyota hao wamekuta rekodi ya mastaa waliofanya vyema na Simba kuchukua mataji ya ubingwa.

“Mkude na Ajibu, wakiondoka hawapunguzi chochote Simba, watasajiliwa wengine wenye kumudu majukumu zaidi yao hivyo wakidhani kuna mtu wanamkomoa wajue kwamba wanakomoa viwango vyao,” alisema.

Mbali na hilo, aliwashauri viongozi wa Simba, kusajili beki wa kulia, beki wa kati na kiungo ambao wataongeza nguvu kwa wale waliopo na kushukuru ujio wa kipa mpya kutoka Ghana,” alisema.

Alisisitiza nyota anayebahatika kucheza Simba na Yanga anapaswa kuhakikisha anaacha rekodi ya kukumbukwa na siyo mladi kuitwa staa.

Kuhusu mabadiliko ya benchi la ufundi la watani wao wa jadi, Yanga, alisema hayapi homa kwani na wao wana kocha Joseph Omog, hivyo wanasubiria ushindani,” alisema.