Lwandamina aikabidhi Yanga kwa Msuva

SIMON MSUVA

Muktasari:

  • Kabla ya mchezo huo, mechi nne zilikuwa zimechezwa visiwani hapa na mabao saba pekee kufungwa, hivyo ushindi huo wa kishindo wa Yanga uliweka rekodi mpya na kuonyesha kuwa timu hiyo pengine imepania kuondoka na taji.

Zanzibar. Yanga imeanza mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa rekodi ya aina yake, jambo ambalo limeibua mshtuko kwa timu zinazoshiriki.

Yanga katika mechi yake ya ufunguzi iliifunga Jamhuri ya Pemba kwa mabao 6-0 juzi yaliyofungwa na Saimon Msuva na Donald Ngoma (mawili kila mmoja), Thaban Kamusoko aliyefunga moja sambamba na Juma Mahadhi.

Kabla ya mchezo huo, mechi nne zilikuwa zimechezwa visiwani hapa na mabao saba pekee kufungwa, hivyo ushindi huo wa kishindo wa Yanga uliweka rekodi mpya na kuonyesha kuwa timu hiyo pengine imepania kuondoka na taji.

Katika mchezo huo, Msuva alihusika katika mabao matatu ya Yanga akifunga mawili na kusaidia moja, jambo ambalo limewavutia viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo na kumpa majukumu makubwa zaidi.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema tayari wamezungumza na Msuva na kumweleza juu ya umuhimu wake ndani ya timu na kumtaka afanyie kazi baadhi ya mapungufu machache katika kiwango chake ili aweze kuwa tishio zaidi.

“Ni mchezaji muhimu, amehusika katika nusu ya mabao yetu na nyumbani pia. Anazidi kupiga hatua siku hadi siku.

“Tumezungumza naye, kuna vitu vichache tumemwambia azifanyie kazi, nadhani tunavyozidi kwenda atakuwa hatari zaidi,” alisema Mwambusi baada ya ushindi huo.

Akizungumzia ushindi wao na Jamhuri, Mwambusi alisema timu yao ilizingatia mafunzo ya kocha na ndiyo sababu walifanya kazi kubwa na kuhakikisha ushindi unapatikana.

Msuva, Ngoma vitani

Msuva na Ngoma na straika wa URA, Bakota Labama wameingia katika vita ya kuwania ufungaji bora na kila mmoja sasa amefunga mabao mawili. Labama aliifungia URA mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya KVZ ya visiwani hapa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Chama Cha Soka Temeke, Omary Chuma alijitolea zawadi kwa ajili ya tuzo hizo jambo ambalo limeibua vita kubwa baina ya wachezaji hao